Serengeti Boys yatwaa ubingwa Chalenji
Muktasari:
- Serengeti Boys imetwaa ubingwa wa Kombe la Chalenji kwa vijana chini ya miaka 17, baada ya kuichapa Somalia kwa mabao 2-0 katika fainali iliyofanyika Bunjumbura, Burundi.
Kocha wa Serengeti Boys, Oscar Milambo amesema ubingwa wa kombe la vijana wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) chini ya miaka 17, ‘Chalenji’ ni ishara njema kuelekea mashindano ya Afcon U17 mwakani.
Serengeti Boys imetwaa ubingwa wa Kombe la Chalenji kwa vijana chini ya miaka 17, baada ya kuichapa Somalia kwa mabao 2-0 katika fainali iliyofanyika Bunjumbura, Burundi.
Bao ya Serengeti Boys yalifungwa na Edson Jeremiah na Jaffary Mtoo kupachika bao la pili na kujihakishia ubingwa huo.
Akizungumzia ushindi huo kocha Milambo alisema "niwapongeza vijana kwa kujituma, pamoja na uchanga wao walicheza vizuri kwa kusikiliza maelekezo yetu, tunaujasiri wa kusema kikosi hiki kinaweza kufanya makubwa kwenye ardhi ya nyumbani.
"Kuchukua kwetu ubingwa ni matunda ya maandalizi ya muda mrefu ambayo tulifanya, tumepata kipimo tosha kwa kuona baadhi ya mapungufu ambayo tutaendelea kuyafanyia kazi ili tuwe na kikosi bora zaidi, " alisema Milambo.
Serengeti Boys ilitinga fainali baada ya kuifunga Kenya mabao 2-1 kwenye hatua ya nusu fainali huku Somalia wakitoka kuifunga Uganda kwa bao 1-0.
Katika mchezo wa kuwania mshindi wa tatu, Uganda imenyakuwa nafasi hiyo baada ya kuifunga Kenya kwa mabao 4-1.