Serengeti Boys waanza vibaya Uturuki

Muktasari:
Mchezo huo ni wa kwanza kwa Serengeti Boys katika mashindano hayo makubwa duniani ya UEFA ASSIST.
Antalya: Kikosi cha timu ya taifa cha vijana chini ya miaka 17 'Serengeti Boys' kimeanza vibaya mashindano ya UEFA ASSIST yanayoendelea nchini Uturuki baada ya kufungwa bao 1-0 na Guinea.
Kocha mkuu wa timu hicho, Oscar Mirambo amesema, wanachukua matokea hayo kama changamoto ya wao kuwa bora zaidi katika mechi zijazo.
"Hatukuwa na kipindi kizuri cha kwanza lakini kipindi cha pili baada ya kufanya marekebisho na kuzungumza na vijana vizuri mambo ya ufundi, walirudi wakiwa vizuri tukamaliza kwa matokeo hayo,"alisema Oscar.
Amesema, kulikuwa na changamoto ya kimazingira katika mchezo huo kama uwanja kuwa na maji, mvua na mambo mengine, wanakwenda kuzifanyia kazi ili hali hiyo itakapotokea kwa mara nyingine isiwasumbue.
Amefafanua kuwa waliingia kipindi cha kwanza wakiwa na malengo ya kuzuia lakini kwenye kiungo mambo hayakwenda sawa: "Viungo walituangusha, tulitaka mmoja acheze chini na mwingine juu lakini mwisho wa siku ikawa tofauti."