Serengeti Boys inazitaka fainali za Dunia

Muktasari:
Kocha huyo wa timu hiyo ya taifa ya vijana wa umri chini ya miaka 17 inayoshiriki michuano maalum la kuwania kufuzu fainali za AFCON U17 kwa 2019 kwa Kanda ya CECAFA, amesema akili yao ni fainali za Kombe la Dunia.
SERENGETI Boys imekuwa ikikonga nyoyo za mashabiki wa soka nchini kwa kazi inayoifanya, lakini kumbe mambo bado kabisa kwa jinsi mipango ya Kocha Mkuu wake, Oscar Milambo, ilivyo.
Kocha huyo wa timu hiyo ya taifa ya vijana wa umri chini ya miaka 17 inayoshiriki michuano maalum la kuwania kufuzu fainali za AFCON U17 kwa 2019 kwa Kanda ya CECAFA, amesema akili yao ni fainali za Kombe la Dunia.
Milambo alisema anatamani na wanajipanga na vijana wake kuhakikisha mwakani wakiwa wenyeji wa fainali hizo za Afrika wafanye vizuri ili washiriki fainali za Kombe la Dunia. Fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wa umri wao mwakani zitafanyikia Peru kati ya Septemba 17 - Oktoba 8.
Akizungumza na Mwanaspoti, Milambo alisema anaamini kama vijana wake watapambana katika fainali hizo za AFCON 2019 basi moja ya nafasi mbili za juu za kundi watakalopangwa itakuwa ni yao.
“Mpaka hivi sasa tushajuana nini tunatakiwa kukifanya, lakini lengo letu katika fainali hizi ni kuhakikisha tunamaliza nafasi nne za juu ili tupata nafasi ya kwenda Kombe la Dunia,” alisema Milambo.
Aliongeza mechi ni ngumu kwelikweli katika kuzipata nafasi hizo kwani kila timu shiriki inazipigia hesabu, lakini watatumia uenyeji wao na kucheza mbele ya mashabiki wao kufaniukiwa.
Katika fainali za 2017 zilizofanyika Gabon, Serengeti ilikosa tiketi za kwenda India katika fainali za Dunia dakika za mwishoni katika kundi lake kwa kupoteza mbele ya waliokuwa watetezi, Mali.
Kikosi hicho juzi Alhamisi, kilipata ushindi wa pili mfululizo katika Kundi A kwa kuinyoosha Sudan kwa mabao 5-0 na kufuzu nusu fainali na Kocha Milambo alisema ujio mpya wa kikosi chake tofauti na walivyocheza mchezo wa kwanza ni mipango ya benchi la ufundi.
Milambo alisema changamoto katika mechi ya awali ilikuwa kubwa kwa vijana wake kwani ilikuwa ni mara ya kwanza kucheza nyumbani, ila alijaribu kuwajenga vijana hao ili kufanya vizuri.
“Matokeo tuliyoyapata tuliyatengeneza kwa sababu tuliwaweka chini watoto na kuwaambia nafasi ambayo tunaipata ndio hiyo hiyo tuitumie,” alisema na kuongeza anataka kuifanya Serengeti Boys ya mwaka huu kuwa bora zaidi ya ile ya mwaka jana.