Sancho? Bebeni hawa watu fasta

MANCHESTER, ENGLAND. GWIJI wa Manchester United, Paul Scholes ameitaka klabu yake hiyo ya zamani kuachana na mpango wa kumsajili Jadon Sancho na badala yake iweke msisitizo kwenye usajili wa Harry Kane au Erling Haaland.

Kocha wa Man United, Ole Gunnar Solskjaer alimworodhesha Sancho kuwa ni chaguo lake la kwanza kwenye usajili wa majira ya kiangazi ya mwaka huu, lakini alishindwa kunasa huduma yake.

Scholes anawataka Man United waweke mkazo kwenye usajili wa ama Kane au Haaland na waachane na Sancho kwa sababu si eneo wanalohitaji kulifanyia mabadiliko, huku akitaka pia wasajili mabeki.”

Scholes alikasirishwa pia na mabosi wa timu kushindwa kumpa sapoti kocha wao Solskjaer kwenye kufanya usajili wa wachezaji anaowahitaji kwa ajili ya kufanya kweli kweli timu.

“Sidhani kama huyu ni mtu wa kwanza kushindwa kupewa sapoti na mabosi. Nadhani (Louis) van Gaal na (Jose) Mourinho walilalamikia jambo hilo, hawakupata wachezaji waliowahitaji,” alisema.

“Kumekuwa na matumizi makubwa sana ya pesa, lakini je yalitumika kwenye wachezaji chaguo la kwanza waliotakiwa na makocha? Sina uhakika huo.”

Hii si mara ya kwanza kwa Scholes kutoa maoni yake akitaka Man United ifanye usajili wa kumnasa Kane.

Mapema mwaka huu, Scholes - ambaye ameteuliwa kuwa kocha wa muda wa Salford City, alisema: “Nadhani tayari tuna wachezaji watatu wanaoweza kucheza pembeni kama Sancho, sidhani kama tunamtaka.”

Man United iliambiwa kwamba Kane anauzwa Pauni 200 milioni huku kocha wa zamani wa Tottenham Hotspur, timu anayochezea straika huyo kwa sasa, Harry Redknapp akisema kwamba suala hilo linawezekana.