Samatta: Wakaushieni hao villa, imetosha

MBWANA Samatta, amezungumza kwa mara ya kwanza na Mwanaspoti tangu atue Fenerbahnce ya Uturuki na kuwasihi mashabiki waache kuisakama Aston Villa mitandao.

Alisema kakutana na wachezaji wapya, timu ngeni, mazingira mageni, lakini anaona ni vitu ambavyo vinazoeleka hivyo anapambana kufanya kazi yake kwa ufanisi mkubwa.

“Changamoto katika maisha mapya ni lazima, ila mazingira yanazoeleka, kikubwa najua nini nakifanya katika majukumu yangu ya soka, huku nikiendelea kuzoea tamaduni zao taratibu,” alisema.

Samatta alipoulizwa ni sababu gani imemfanya auzwe Fenerbahce akajibu: “Katika soka kuna mambo mengi ambayo mashabiki ni vigumu kuyaona hivyo, yanabakia kwa mchezaji na waajiri wake.

“Kwa sasa nitaendelea kukaa kimya kwani bado ninacheza, hivyo sio busara kuanza kuongea ongea, ila ipo siku nitatafuta muda wakuyaweka wazi yote, naamini nitakuwa nimeyajibu maswali ya wengi,” alisema Samatta na aliongeza kuwa.

“Huu ni muda wangu wa kufanya kazi, nikimaliza soka nitakuwa na mengi ya kuzungumza ambayo yatawafunza wengine ama kuwatia moyo wa kupambania ndoto zao ili waweze kuziishi kwa vitendo,” alisema.

SIKIA OMBI LAKE

Huko kwenye mitandao ya kijamii kuliwaka moto wakati Samatta akielekea zake Uturuki, lakini mwenyewe amewaomba waachane na jambo hilo, ili lisije likazuia riziki za wanasoka wengine wa Tanzania kusajiliwa ndani ya kikosi hicho.

Alisema kuna vipaji vingi nchini na kuna siku Mtanzania mwingine anaweza kukipiga Villa, lakini kwa yanayoendelea yanaweza kuleta shida.

“Ndio maana tangu mwanzo nimesema kuna mambo mengi, ambayo hata mimi ningeongea sana, ila sio muda wake, tuwe na subra. Acheni kuwaandama Aston Villa mitandaoni ili tuzidi kupanua wigo wa vijana wetu kuja kucheza huko baadaye. Wasituone sisi wakorofi wataogopa kuchukua wachezaji wa Kitanzania,” alisema.