Samatta aondoa gundu Fenerbahce

Samatta aondoa gundu Fenerbahce

Muktasari:

  • BAADA ya ukame wa muda mrefu wa mabao akiwa na kikosi cha Fenerbahce hatimaye staa Mtanzania na Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta amefuta gundu kwa kuifungia timu hiyo bao la ushindi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Uturuki dhidi ya Denizlispor, juzi Jumatatu.

BAADA ya ukame wa muda mrefu wa mabao akiwa na kikosi cha Fenerbahce hatimaye staa Mtanzania na Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta amefuta gundu kwa kuifungia timu hiyo bao la ushindi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Uturuki dhidi ya Denizlispor, juzi Jumatatu.

Samatta kabla ya kufunga kwenye mechi hiyo alishacheza mechi 11 bila ya kuonja ladha ya bao, mara ya mwisho kufunga ilikuwa ni Januari 25, mwaka huu kwenye mchezo dhidi ya Kayserispor.

Kabla ya mechi hiyo Denizlispor haikuwa imepata ushindi kwenye mechi tatu mfululizo na baada ya kutembelea dimba la Sukru Saracoglu Stadium, imeendelea na rekodi hiyo mbaya kwa kucheza mechi nne sasa bila ya ushindi.

Baada ya kuihakikishia ushindi timu yake, Samatta alitolewa nje dakika ya 90 nafasi yake ilichukuliwa na Mert Hakan Yandas.

Ushindi huo umeiwezesha Fenerbahce kufikisha alama 62 kwenye mechi 31 na kupanda hadi nafasi ya pili nyuma ya kinara Besiktas ambayo ina alama 64 na faida ya mchezo mmoja mkononi.

Tangu ajiunge na wababe hao katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana, Samatta amecheza mechi 27 za michuano yote na kufunga mabao sita.