Samatta, Aboubakar, wachonganishwa Uturuki

Monday September 28 2020
samatta pic

NAHODHA wa timu ya taifa la Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta ambaye kwa sasa anaichezea klabu ya Fenerbahce S.K ya nchini Uturuki, amechonganishwa huko na mshambuliaji mwenzake wa Kiafrika Vincent Aboubakar anayeichezea Besiktas.

Samatta na Aboubakar ambaye ni Mcameroon, wamechonganishwa na mtandao wa Twitter wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ambao ulitupia picha zao huku wakitoa nafasi ya wadau kupiga kura kuwa nani atatisha msimu huu wa Ligi Kuu Uturuki ‘Super Ligi’.

CAF walitupia posti hiyo, Septemba 26 na aliyeonekana kuongoza hadi jana saa sita kabla ya muda wa kushindanishwa kumalizika, alikuwa Samatta ambaye alikuwa akiongoza kwa kupigiwa kura nyingi.

Samatta alipata asilimia 62.7% ya kura 119,458 zilizopigwa huku mpinzani wake Aboubakar akiwa na asilimia 37.3% ya kura hizo.

Kwa upande wa wadau ambao waliamua kusema chochote kwenye posti hiyo, asilimia kubwa walionekana kumsifia Samatta wakisema kiwango chake ni kikubwa kuliko Aboubakar ambaye kabla ya kujiunga na Besiktas alikuwa akiichezea FC Porto ya Ureno.

Miongoni mwa wadau hao ni mchambuzi wa soka nchini, Geoffrey Lea alisema, “Aboubakar sio wa kiwango cha Samatta, Samatta atapigania kiatu cha ufungaji bora tena kirahisi tu.”

Advertisement

Murat Gok ambaye ni Mturuki, alisema wakati akiwa KRC Genk ya Ubelgiji, Samatta aliwahi kuinyoosha Besiktas kwa kufunga mabao mawili hivyo ni dhambi kumfananisha nyota wao huyo mpya na washambuliaji wa ajabu, “Ni vizuri kumheshimu Samatta, atatubeba msimu huu.”

Mbunge Tarime Vijijini 2030, Dadydony alisema, “Mna masihara nyie. Tanzania haijawai kushindwa kwenye mambo ya mitandaoni. Mwekeni hata Messi na Samatta halafu mtuulize nani mchezaji bora muone kama Samatta hajaibuka mshindi.”

Kwa mujibu wa mafanikio ambayo kila mmoja ameyapata kwenye uchezaji wao soka, Aboubakar mwenye miaka 28 ametwaa mara moja Kombe la Mataifa ya Afrika akiwa na Cameroon.

Akiwa na FC Porto ambako mambo yalimshinda na kutolewa kwa mkopo alitwaa mataji manne ambayo ni Ligi Kuu Ureno ‘Primeira Liga’ mara mbili, Ngao ya Jamii ‘Super Cup’ mara moja na Kombe la Ligi mara moja.

Baada ya kupoteza nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha FC Porto ndipo alipotolewa kwa mkopo kuichezea Besiktas na kutwaa taji moja la Ligi Kuu nchini humo msimu wa 2016/17 huku akifunga mabao 12 kwenye michezo 27 ya ligi hiyo maarufu kama Super Ligi.

Aboubakar ni mchezaji rasmi Besiktas ambaye amesajiliwa Septemba 25, 2020 kwa ada ya Euro 5 milioni.

 

 

Advertisement