Saliboko aizamisha Mtibwa Sugar

Muktasari:

  • Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa ulishuhudia Saliboko akifunga bao hilo dakika ya 56 baada ya kupiga shuti kali lililomshinda kipa wa Mtibwa, Justine Ndikumana na kuiwezesha KMC kufikisha pointi 32 nyuma ya Coastal Union walioko nafasi ya nne wenye pointi 33.

Kiungo mshambuliaji wa KMC, Daruweshi Saliboko amelizamisha jahazi la Mtibwa Sugar baada ya kufunga bao pekee la ushindi katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa leo kwenye Uwanja wa Manungu,Turiani mkoani Morogoro.

Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa ulishuhudia Saliboko akifunga bao hilo dakika ya 56 baada ya kupiga shuti kali lililomshinda kipa wa Mtibwa, Justine Ndikumana na kuiwezesha KMC kufikisha pointi 32 nyuma ya Coastal Union walioko nafasi ya nne wenye pointi 33.

Mchezo huo uliokuwa muhimu kwa Mtibwa Sugar kutetea matumaini ya kubaki Ligi Kuu msimu ujao, lakini timu hiyo imeshindwa kufurukuta mbele ya Watoza ushuru wa Kinondoni.

Mshambuliaji wa Mtibwa, Charles Ilanfya alikosa mkwaju wa penalti  dakika ya 55 baada ya mpira kumgonga kwenye mkono wa beki wa KMC, Andrew Vicent licha ya jimyson Mwanuke kuurudisha golini bado uliokolewa.

KMC kwa msimu huu inakuwa mbabe wa Mtibwa kwa kupata alama zote sita katika michezo miwili ya ligi waliyocheza ambapo mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Mtibwa walifungwa pia bao 1-0.

Baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Kocha wa KMC, Abdilhamid Moalin  amesema timu yake imecheza chini ya kiwango kipindi cha kwanza, lakini cha pili wakaja kivingine na kupata matokeo

"kipindi cha kwanza tumecheza chini ya kiwango, tulivyoenda mapunziko nikawaambia wachezaji kwamba tucheze kwenye mipango yetu ili tupate kile tunachotaka, nafurahi kipindi cha pili wamecheza vile ambavyo tumeelekezana tumetengeneza nafasi nyingi na tumepata matokeo, nadhani wao (Mtibwa) walicheza kipindi cha kwanza na sisi kipindi cha pili"

Kwa upande wake, Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila amesema mipango ilikuwa kushinda,

 "Imetuuma kukosa hizi alama, huu mchezo ungetuweka kwenye nafasi nzuri, lakini imetugharimu sana kwenye hizi mechi nane zilizobaki tutakaa chini tujadili wapi tumekosea ili twende mbele. Kazi kubwa iliyopo ni kuwaweka sawa kisaikolojia wachezaji maana bado tuna mechi za kucheza na sijafurahishwa na kiwango," amesema Katwila.

"Wachezaji bado matarajio yapo ya kubaki kulingana na timu zilivyobanana kwa pointi, hivyo tutapambana ili timu ibaki (Ligi Kuu) na tukikosa kabisa tucheze 'play off," amesema Katwila.