Sakho atoa ahadi nzito, afichua walivyokaa kikao kizito

WINGA wa Simba, Pape Ousmane Sakho ameshusha mkwara kwamba wao kama wachezaji wana jambo lao zito na kwamba mchezo wa Aprili 3 dhidi ya Union Sportive de la Gendarmerie utarudisha heshima yao na ndicho walichokubaliana kwa pamoja kikaoni.
Akizungumza na Mwanaspoti, Sakho alisema baada ya timu yao kupoteza dhidi ya ASEC Mimosas walikutana kama wachezaji kisha kukubaliana kwamba wana deni kwa mashabiki wao haswa kwenye ardhi ya Dar es Salaam.
Sakho alisema watakaporudi kazini baada ya mapumziko ya siku chache watakuwa na umakini mkubwa kuhakikisha wanarudia tena maajabu yao ya kufuzu hatua ya robo fainali wakitumia Uwanja wa Mkapa.
“Tumekutana kama wachezaji na niseme Simba hatujatoka katika mashindano ila tumepoteza moja ya mechi na tumeumia kwa matokeo yale,”alisema Sakho ambaye mechi mbili za wekundu hao nyumbani ametupia kila mechi bao moja tena makali.
“Tukirudi kambini kama wachezaji tumekubaliana kwamba tunatakiwa kurudisha heshima yetu kupitia mchezo wa Gendarmerie naiona Simba ikifuzu tena kupitia uwanja wa nyumbani,” aliongeza.
Sakho alisema makocha wao wameona wapi walikosea kupitia mchezo wa ASEC lakini pia wanawajua vyema Gendarmerie ambao walitoka nao sare ugenini ya bao 1-1 na kwamba watajua ni aina gani ya maandalizi wanayahitaji kuelekea mchezo huo.
“Sisi kama wachezaji tumeshajiandaa kiakili lakini makocha nao wanajua maandalizi gani yanahitajika kuelekea hiyo mechi, Gendarmerie tunawajua na wao wanatujua lakini kitu ambacho wanakuja kukutana nacho wanakuja kujua ubora wetu tunapokuwa mbele ya mashabiki wetu.”
Simba inahitaji ushindi katika mchezo huo ili ifuzu hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho huku ikisubiri timu moja kati ya Berkane au ASEC ambao watakutana katika mchezo mwingine nchini Morocco.
PABLO ANENA
Wachezaji wa Simba wamepewa mapumziko ya siku tano na wanarejea kambini Machi 27, watakula chakula cha mchana kwa pamoja kabla ya saa 10:00 jioni kuanza mazoezi.
Mapumziko ya wachezaji wa Simba yalianza Machi 22, mara baada ya kutua nchini kutokea Benin kila mchezaji aliruhusiwa kwenda kwake na wengine walikuwa na majukumu ya timu za taifa kama kipa, Aishi Manula ingawa uongozi umesisitiza ndani ya hizi siku 10 kila kitu kitakuwa sawa.
Kocha wa Simba, Pablo Franco alisema; “Baada ya kurejea kambini tutakuwa na wiki moja hivi ya kufanya maandalizi naimani inatutosha kwetu kwa kila mchezaji kufanya kile kinacho hitajika na kufanya vizuri katika mchezo wa USGN.”
“Malengo makubwa ni kufuzu katika hatua inayofuata kutokana na kiu ya mafanikio tuliyokuwa nayo naimani kubwa hilo linawezekana ingawa tutakuwa na mechi ngumu kutokana na wapinzani wetu nao wananafasi kama ya kwetu.” Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ amesisitiza kwamba kila kitu kiko kwenye mipango na wanaelewa kiu ya mashabiki ni kufuzu .