SAIDO: Kama vipi waleteni hao Simba!

Monday May 03 2021
SAIDO PIC
By Khatimu Naheka

KIKOSI cha Yanga kilirejea juzi jijini Dar es Salaam kikitokea Sumbawanga, huku ushindi wa wa bao 1-0 ilioupata Yanga dhidi ya Tanzania Prisons ukiwaongeza mzuka na sasa akili wameelekeza kwenye pambano lao dhidi ya Simba, huku mshambuliaji nyota, Said Ntibazonkiza ‘Saido’ akichimba mkwara akisema, “hao Simba na waje tu sasa.”

Kama ilikupita hii ni kwamba, Yanga ilishinda katika mchezo wa Kombe la Shirikisho (ASFC) na kutinga robo fainali, na kipigo hicho ni cha kwanza kwa Yanga dhidi ya Prisons, lakini ushindi huo umefanya Saido pamoja na Kocha wake, Nasreddine Nabi kupiga mkwara kwa Simba.

Akizungumza na Mwanaspoti, Saido alisema ushindi umewarudishia morali kwa kiasi kikubwa wakati wakirudi kambini kuanza kujiandaa na Simba na sasa acha waje wakutane nao wamalize.

“Huu ni ushindi muhimu katika mechi ngumu, kwa sasa niseme morali imerejea kwa nguvu na tupo tayari kukutana na Simba, ni hatua nzuri unapokwenda kukutana na mpinzani wako ukiwa unatoka kushinda hasa mechi kama hii ambayo ushindi wake ulikuwa mgumu kupatikana,” alisema.

Achekelea mbinu za Nabi

Akizungumzia ushindi wa kwanza wa Nabi, Saido alisema taratibu anaona mabadiliko katika ubora wa kikosi chao ambapo sasa wanaweza kuwa bora kutengeneza mashambulizi vizuri na hata kuzuia kwa nidhamu kubwa wakati kocha wao huyo raia wa Tunisia akiwa na mchezo wa pili pekee.

Advertisement

Saido alisema kwa nafasi kubwa wachezaji wenzake wameanza kuelewa mbinu za Nabi hatua ambayo juzi iliwasaidia kushinda mchezo mgumu dhidi ya Prisons.

Mshambuliaji huyo mkongwe raia wa Burundi alisema Nabi kama atapewa siku 10 za utulivu kuendelea kuingiza mbinu zake kuna nafasi kubwa ya kuirejesha Yanga katika ubora wa kushinda akisema pia ushindi huo wa juzi umewarudishia morali kwa kiasi kikubwa.

“Tumeanza kuona mabadiliko, ukiangalia tunavyocheza sasa na mechi chache za kabla ya ujio wake kuna kitu tofauti utakiona kuhusu ubora, timu imetulia na inatengeneza nafasi, tulikuwa bora sana leo (juzi) kuliko wapinzani wetu, tulistahili kitu tofauti,” alisema mtoa pasi ya bao la mchezo wa juzi.

“Kocha (Nabi) ameanza vizuri nafikiri anahitaji kama siku 10 kutoka sasa watu kuona mabadiliko makubwa zaidi, mashabiki wanatakiwa kumuunga mkono na kuiunga mkono timu yao, naona kuna mambo makubwa hapa yatakuja kupatikana kama tutaendelea na mwendo huu wa kushinda ambao kocha anataka tufanye,” alisema Saido.

“Huu ni ushindi muhimu kwa timu ukizingatia tuliwahi kuja hapa tukakutana na ugumu wa kushinda, lakini wengi wamekuwaa wakishindwa kushinda, sasa morali yetu imerudi kuwa juu zaidi kuelekea mechi zijazo za ligi.”

NABI HUYU HAPA

Akizungumzia ushindi huo, Nabi, aliwapongeza wachezaji wake kwa kupambana na kushinda mchezo huo akisema taratibu vijana wake wameanza kuimarika na kushika anachotaka.

Nabi alisema sasa wanarudi kambini kuanza haraka maandalizi ya mchezo ujao dhidi ya Simba na kwamba, anatambua mechi hiyo itakuwa ngumu huku akigoma kufunguka kwa undani ubora wa watani wao hao wa jadi.

“Naona vijana wangu wanaimarika, nimefurahi kuona kila mchezaji akicheza kwa morali kubwa,kama wachezaji wanaotakiwa kuipigania Yanga, nafurahi kuona wameanza kushika kile ninachotaka wafanye ingawa bado kuna kazi kubwa inatakiwa kuendelea kufanyika,” alisema Nabi.

“Najua tunakwenda kucheza mchezo mgumu na timu yenye upinzani mkubwa, tunawaheshimu Simba, ni timu yenye ubora, lakini nafikiri itakuwa ni mechi ya tofauti leo (juzi) tuliwakosa wachezaji wetu wanne, naamini wapo ambao watakuwa wamerejea katika mechi hiyo, sasa tutaingia katika maandalizi.”

Advertisement