Sababu mbili Okrah kuondoka Simba zaanikwa

Dar es Salaam. Klabu ya Simba tayari imetangaza kuachana na kiungo mshambuliaji wake, Augustine Okrah, ambaye amedumu kikosini kwa msimu mmoja.

Taarifa iliyotolewa na Simba kupitia ukurasa wake wa Instagram ilisema: "Baada ya kuwa kwenye kikosi chetu kwa msimu mmoja, Augustine (Okrah) hatakuwa sehemu ya timu yetu msimu ujao."

Upande wake kupitia mtandao huo huo, Okrah aliandika: "Maisha ya kazi yetu ni kuwa na watu wanaokuja na kuondoka, watu wa kukumbukwa kwa walionifanya niwe hapa, nitazidiki kuwakumbuka.

"Mazuri yote tuliyokuwa nayo, nitawamiss wote na ahsanteni sana kwa jambo letu tukawa pamoja na naomba kazi yetu itukutanishe tena, ahsanteni Simba, mashabiki wa Simba, mashabiki wangu na ahsante Tanzania."

Awali, gazeti mama na hili (Mwanaspoti) liliwahi kuandika kuwa Okrah ameomba kuondoka kwa kuandika barua katika timu hiyo kutokana na sababu mbili, ikiwemo ugonjwa wake wa kushindwa kupanda ndege mfululizo na lingine ni kutokuwa na maelewano mazuri na baadhi ya viongozi kwenye benchi la ufundi.

Kawaida, Simba huwa inatumia usafiri wa ndege kucheza mechi zake hata hapa za ndani, jambo ambalo kwa Okrah ni gumu kwani akipanda ndege inabidi asubiri muda ili akae sawa.

Rafiki wa karibu na mchezaji huyo alilidokeza Mwananchi kwamba Okrah akipanda ndege anatakiwa asubiri kwa muda usiopungua siku mbili ili kurejea kwenye hali yake ya kawaida.

"Kwa ratiba za Simba ilikuwa ni changamoto kwake kwa sababu akiwa angani inamuhitaji muda usiopungua siku mbili kurejea kwenye hali yake ya kawaida.

“Si yeye tu, kuna watu wengi duniani hawapandi ndege kutokana na tatizo hilo, kuna wengine hawavuki maji na wengine hawapandi hata mabasi, hilo linatokea na kwa Okrah ndege ni changamoto," alisema rafiki huyo.

Jambo lingine ambalo Mwananchi limeambiwa juu ya mchezaji huyo ni kwamba Okrah hana maelewano mazuri baadhi ya watu katika benchi la ufundi la Simba chini ya kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’.

Kutokana na hali hiyo, iliufanya uongozi wa Okrah kuanza kumtafutia timu nyingine winga huyo, kwani unaamini licha ya kutaka kuondoka, lakini pia hayupo kwenye mipango ya benchi la Simba kwa msimu ujao chini ya Robertinho.

Simba ilimsajili Okrah kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Bechem United ya Ghana kwa Dola 200,000 (sawa na Sh460 milioni), akiwa bado na mwaka mmoja, wakati huo akiwania na Yanga na timu nyingine ya Uarabuni.