Saa 72 za moto kwa Kaze

Thursday February 25 2021
72 pic
By Khatimu Naheka

YANGA itarudi uwanjani kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Ken Gold itakayopigwa wikiendi hii, kisha itahamishia akili na nguvu katika mechi mbili za ugenini zitakazochezwa ndani ya saa 72, ila rekodi za viwanja hivyo zinamtega Kocha Cedric Kaze.

Jumamosi itaingia kwenye vita ya ASFC ikiwa Uwanja Uhuru kuikaribisha Ken Gold, lakini baada ya mechi itarudi kwenye ligi ambako wamesisitiza msimu huu lazima kieleweke.

Mchezo wa kwanza utakuwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga watakapowafuata Coastal Union katika mechi itakayopigwa Machi 4 na siku tatu baadaye itasafiri hadi Moshi kuumana na Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Ushirika.

Katika mechi hizo zote mbili lolote linaweza kutokea kutokana na kuwa viwanja vigumu kwa Yanga, ambako msimu uliopita iliambulia sare kotekote, huku mchezo wa Moshi ukihitaji huruma ya marefa kuwaokoa Yanga kwenye kipigo mbele ya maafande wa Polisi.

Mara ya mwisho kushinda Mkwakwani ilikuwa Februari 3, 2015 waliposhinda kwa bao 1-0 lakini baada ya hapo wakatoka sare mbili mfululizo kisha nyuma kidogo walilala mabao 2-0.

Ingawa Yanga imekuwa ikijipigia Coastal Union wanapokuwa Dar es Salaam, lakini hesabu zao hutibuliwa wanapokutana Tanga.

Advertisement

Achana na mechi ya Tanga, Yanga itaifuata Polisi ambayo msimu uliopita iligoma kupoteza mechi kwa vinara hao wa msimu huu, kwani walitoka sare ya 3-3 jijini Dar es Salaam na mechi ya marudiano Moshi iliisha kwa sare ya 1-1, huku Polisi wakikataliwa bao jingine.

Rekodi za viwanja hivyo viwili ndizo jana zilisababisha mabosi wa Yanga kuitisha kikao cha dharura wakizijadili, hasa ikizingatiwa mechi zao tatu zilizopita dhidi ya Mbeya City, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar, Yanga ilipata pointi tano za jasho na damu.

Mshauri wa Uongozi wa Yanga, Senzo Mazingisa ameliambia Mwanaspoti wanatambua ugumu katika mechi zao na kwamba, wamekuwa na mikakati mizito kuhakikisha wanaondoka na pointi zote sita.

Senzo alisema benchi la ufundi linatambua ugumu wa viwanja hivyo, akisema: “Hakuna mchezo rahisi kwa Yanga, kila mechi imekuwa ngumu kwetu lakini tunajua ugumu huo na tunajipanga kwa kila hatua kuhakikisha hatuharibu hesabu zetu katika mechi hizo na zingine.”

“Makocha wetu wanafanya kazi zao kwa umakini katika kuandaa kikosi chetu, tunafurahi kwamba wapo baadhi ya wachezaji wameanza kurejea kutoka katika majeruhi wakati tunaelekea kwenye mechi hizo, hii kwetu ni kama taarifa ya kutupa gia yenye nguvu.

“Kitu muhimu ni mashabiki wetu wapo ambao wanasafiri na wengine ambao kila tunapokwenda waje kwa wingi kuwapa morali wachezaji wao.”

Katika mechi ya awali msimu huu iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Yanga ilishinda mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union iliyokuwa ya mwisho kwa kocha Zlatko Krmpotic kabla ya kumpisha Kaze aliyeiongoza Yanga kuinyoosha Polisi kwa bao 1-0.

Advertisement