Ruvu Shooting yaanza kupapaswa

Tuesday September 28 2021
ruvu pic
By Daudi Elibahati

KLABU ya Dodoma Jiji imeanza vyema Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0, dhidi ya Ruvu Shooting katika Uwanja wa Jamhuri.

Bao pekee la Dodoma lilifungwa na kiungo mshambuliaji wa timu hiyo Cleophance Mkandala dakika ya 33 ya kipindi cha kwanza baada ya kupiga shuti kali nje ya 18 na kumshinda golikipa wa Ruvu Shooting Mohamed Makaka.
 
Dodoma ilionekana kumiliki mchezo katika kipindi cha kwanza huku ikikosa umakini kwenye umaliziji wa nafasi na kuwapa wakati mgumu Ruvu Shooting ambayo ilikosa muunganiko mzuri kuanzia eneo la kiungo mpaka ushambuliaji ambalo lilikuwa likiongozwa na Elias Maguri.

Kipindi cha pili timu zote zilionekana kushambuliana kwa zamu huku zikitengeneza nafasi kadhaa ambazo walishindwa kuzitumia, hivyo wenyeji kutumia vyema Uwanja wao wa nyumbani.

Matokeo haya yanaifanya Dodoma Jiji kuendelea kuwa wababe wa Ruvu Shooting kwani tangu timu hiyo ipande Ligi Kuu Bara msimu wa 2019/20, imeendelea kupata matokeo ya ushindi.

Mara ya mwisho kwa timu hizi kukutana katika Uwanja wa Jamhuri ilikuwa ni Octoba 2, Mwaka jana kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo Dodoma Jiji iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Advertisement