Robertinho achekelea kutemwa Kapombe

Muktasari:

  • Mabeki hao wawili wanaocheza pembeni, kulia na kushoto licha ya kuwa kwenye kiwango bora kwa sasa lakini hawakujumuishwa Taifa Stars kwa sababu ambazo hazijawekwa wazi na kocha mkuu wa timu hiyo Adel Amrouche licha ya kuonekana akiongea nao wikiendi hii Uwanja wa Benjamin Mkapa.

KITENDO cha mabeki tegemeo wa Simba, Shomari Kapombe na Mohamed Hussein 'Tshabalala' kutojumuishwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars dhidi ya Uganda kimempa mzuka kocha mkuu wa Simba, Roberto Oliveira 'Robertinho' anayeamini atapata muda zaidi wa kuwanoa.
Stars ipo kambini Misri ikijiandaa na mechi mbili za kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (AFCON 2023).

Mabeki hao wawili wanaocheza pembeni, kulia na kushoto licha ya kuwa kwenye kiwango bora kwa sasa lakini hawakujumuishwa Taifa Stars kwa sababu ambazo hazijawekwa wazi na kocha mkuu wa timu hiyo Adel Amrouche licha ya kuonekana akiongea nao wikiendi hii Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Akizungumza na Mwanaspoti Robertinho alisema kwa ubora wa Kapombe na Tshabalala anaona walifaa kuwa kwenye kikosi cha Stars lakini kama hawapo pia siyo mbaya kwani ni maamuzi ya benchi la Stars na sasa atatumia muda huu kukaa nao zaidi pamoja na kikosi chake kuendelea na maandalizi.

Kocha huyo Mbrazil baada ya Simba kuichapa Horoya na kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, alitoa mapumziko ya siku tano kwa wachezaji wake kabla ya kurudi kambini kujiandaa na mechi ijayo dhidi ya Raja Casablanca ugenini Morocco.

"Kapombe na Hussein (Tshabalala), ni wachezaji wazuri na wanaweza kucheza timu yeyote katika ukanda huu, kutoitwa kwao kwenye timu ya taifa siwezi kulizungumzia sana kwani ni maamuzi ya benchi la ufundi na sitaki kuwaingilia kwani nawaheshimu wote," alisema Robertinho na kuongeza;

"Nafurahi kuwa nao na kwa wakati huu ambao ligi zimesimama nitautumia kuwanoa pamoja na wachezaji wengine kuhakikisha tunajenga timu imara kwa kufanyia kazi makosa tuliyonayo na kuboresha kila eneo katika timu yetu."

Aidha kocha huyo aliweka wazi kuisoma Raja na kusema huenda kukawa na mabadiliko kwenye kikosi chake katika mechi hiyo itakayopigwa Aprili Mosi mwaka huu kwani tayari wamefuzu na sasa wanawaza zaidi robo fainali.

"Tumefuzu lakini hatujamaliza, tuna mechi ya mwisho na Raja ambayo tumepanga kucheza kitofauti kidogo na maandalizi yanaendelea baada ya hapo tutaanza hesabu kamili za hatu ya robo fainali.

"Mpira wa miguu ni mchezo wa wazi, hatumuhofii yeyote katika hatua hii bali tunaheshimu timu zote za Afrika na tuko tayari kupambana na yeyote tutakayepangwa nayo," alisema Robertinho.