Refa Ikambi, Simba na Yanga kulikoni!
Simba inaomboleza msiba wa kipigo chao cha kwanza msimu huu katika Ligi Kuu Bara lakini mwamuzi aliyechezesha mechi hiyo ameweka rekodi ya pili katika kuchezesha mechi za maumivu katika klabu kubwa mbili nchini.
Simba juzi Januari 17 imepoteza mechi yake ya kwanza kwenye ligi wakiwa ugenini dhidi ya wenyeji Mbeya City kwa bao 1-0 katika Uwanja wa Sokoine Mkoani Mbeya.
Mchezo huo ulisimamiwa na mwamuzi Raphael Ikambi kutoka Morogoro umeharibu rekodi ya kutofungwa kwa mabingwa hao watetezi.
Ikambi pia msimu uliopita alisimamia mchezo wa kusitisha rekodi ya kutofungwa kwa Yanga dhidi ya Coastal Union Machi 4, 2021.
Yanga ilipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union ukiwa ndio mchezo wao wa kwanza kupoteza msimu huo baada ya kumaliza nusu msimu bila kufungwa.
Rekodi nyingine kwa Ikambi katika mechi hizo ni kwamba alitoa penalti kisha klabu hizo kongwe wakashindwa kuzitumia.
Katika mechi ya Yanga aliyekuwa winga wao Mkongomani Tuisila Kisinda alikosa mkwaju wa penalti ingawa baadaye alikuja kufunga bao pekee la kuitanguliza timu yake kisha Coastal Union kurudisha na na kupata bao la ushindi.
Mechi ya Simba nayo mshambuliaji Mkongomani Chris Koppe Mugalu alipoteza mkwaju wa penalti ukigonga mwamba na kuipotezea nafasi timu yake kusawazisha.