RC Mwanza akoleza mzuka Pamba

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akifanya mazoezi na wachezaji wa timu ya Pamba Jiji kuelekea mchezo wa kesho Ligi ya Championship dhidi ya FGA Talents utakaochezwa uwanja wa Nyamagana jijini humo saa 10 jioni. Picha na Anania Kajuni
WAKATI Pamba Jiji ikitarajiwa kushuka uwanjani kesho kucheza mechi ya mwisho ya Championship ikiwa nyumbani dhidi ya FGA Talents, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amewaongezea mzuka mastaa wa timu hiyo kwa kuwaibukia na kufanya nao mazoezi kisha kuwapa ahadi tamu kama itashinda.
Mtanda aliyekabidhiwa ofisi na aliyekuwa Mkuu wa mkoa huo, Amosi Makalla Aprili 6 katika kikao chake cha kwanza na timu hiyo leo kwenye Uwanja wa Nyamagana amefanya mazoezi na timu hiyo kuanzia saa 3:00-4:00 asubuhi kisha akazungumza na benchi la ufundi na menejimenti ya timu hiyo.
Akizungumza na wachezaji baada ya mazoezi, Mtanda aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara na mlezi wa Biashara United, amewatoa wasiwasi wachezaji akiahidi kuendelea kutoa motisha, kuendeleza mipango iliyoachwa na Makalla huku akiahidi kuanza mikakati mapema ya mechi mbili za mwisho ugenini.
"Nimekuja kuona mazoezi ya timu na kuwahakikishia misheni hii haiwezi kuishia nusu, lazima ikamilike wananchi wa Mwanza wanataka kuiona Pamba Jiji inarudi kule ilikokuwa. Mimi sijaja hapa kuanza upya nimekuja kuendelea pale na mtangulizi wangu ameachia," amesema Mtanda.
"Hapa Nyamagana ni nyumbani hatakiwi kutoka mtu sisi hatuna matokeo mengine tunayoyatarajia ni ushindi tena siyo ushindi mwembamba ni ushindi wa kishindo lakini zile motisha zote ziko palepale na zinapatikana kwa wakati kwahiyo msiwe na wasiwasi."
"Mechi zote zilizobaki tutatumia nguvu ya 'supersonic' kama huko nyuma motisha ilikuwa asilimia 50 basi itafikka asilimia 100. Kesho ninawatakieni kila la kheri na mimi nitakuwepo, tunakuja kupata burudani na kupata matokeo," amesema Mtanda.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Trivonia Kisiga amewataka wachezaji kuyafanyia kazi maelekezo yote ambayo yametolewa na Mtanda huku akisisitiza yote yaliyoahidiwa yatatekelezwa, huku mchezaji wa zamani wa Pamba, Fumo Felician alikazia kwa kusema;"Hii ni neema ambayo tumepata msimu huu kuwa na Amos Makalla na Said Mtanda wote ni wanamichezo, naamini mwaka huu mvua inyeshe jua liwake tutakwenda Ligi Kuu."
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji, Haruna Chanongo amesema; "Kipindi kama hicho tunaangalia mikakati ya kumaliza ligi, kitu kikubwa tunachozungumza kama wachezaji ni kutobweteka kwa sababu safari bado haijaisha mpaka tufanikishe mipango yetu ya kuipandisha timu."