Prisons waendelea kujifua, kukipiga na Ihefu

Muktasari:

Mazoezi hayo ni kwa ajili ya kujiandaa na mwendelezo wa Ligi Kuu inayotarajia kuendelea Oktoba 16 kwa baadhi ya mechi, huku Wajelajela hao wakishuka dimbani Oktoba 19.

Mbeya. Wakati Ligi Kuu ikiwa imesimama kwa muda kupisha kalenda ya kimataifa, huko Tanzania Prisons haijatulia na inaendelea kujifua kwa ajili ya mwendelezo wa michuano hiyo.

Prisons ambayo imeanzia ugenini mechi mbili haijaonja ladha ya pointi tatu baada ya kupoteza mchezo mmoja dhidi ya Mbeya City na kutoa suluhu dhidi ya Mtibwa Sugar.

Kwa sasa timu hiyo inajiandaa na mechi yake dhidi ya Biashara United itakayopigwa uwanja wa Nelson Mandela mkoani Rukwa Oktoba 19 ikiwa ni mchezo wao wa kwanza nyumbani, japokuwa zipo zipo taarifa za kusogezwa mechi hiyo kufuatia maombi ya Biashara United na ratiba yao kimataifa.

Katika mazoezi ya leo chini ya benchi lao la ufundi likiongozwa na Kocha Mkuu, Salum Mayanga zaidi walijikita kusaka pumzi, kufunga mabao na stamina.

Hata hivyo baada ya mazoezi hayo, timu hiyo kesho Jumanne itakuwa uwanjani kukipiga na Ihefu huko wilayani Mbarali katika mchezo wa kirafiki.