Popat wa Azam FC aula Olimpiki maalum

MKURUGENZI wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat' ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Olimpiki Maalumu nchini (Special Olympics Tanzania, SOT), uteuzi uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Popat ameupokea uteuzi huo baada ya Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi (TPLB), Nassor Idrissa 'Father' kumaliza muda katika nafasi hiyo aliyoitumikia kwa kipindi cha miaka tisa.

Kabla ya kuula, Popat alikuwa ni Makamu Mwenyekiti wa bodi hiyo nafasi ambayo kwa sasa inachukuliwa na  mwanamichezo mashuhuri hapa nchini, Mharami Mchume.

"Natumia nafasi hii kutoa shukrani zangu za dhati kwenu wote wajumbe wenzangu  wote kwa pamoja , ni kizuri cha maisha yangu tukiwa pamoja nimejufunza mengi toka kwenu na hasa lililo kubwa zaidi ni mioyo yenu ya kujitolea kwa ajili hawa watoto wetu, mmekua walimu wazuri kwangu na ushirikiano mlionipa tangu nikiwa mjumbe kisha makamu Mwenyekiti hadi nafasi ya juu mliyonipa ya kuwa Mwenyekiti niseme tu kua "asanteni sana " alisema Father na kuongeza;

"Namuomba Mungu azidi kukupeni busara hekima na upendo ule mlionipa mimi pia mumpe Mwenyekitii wetu mpya na makamu wake, niwatakie kila la kheri na mafanikio ili tuendeleze taasisi yetu

Mimi bado tupo pamoja kwa namna yeyote."

Kwa upande wa Popat alishukuru kuipata nafasi hiyo na kuahidi utendaji wa ushirikiano kutoka kwa wajumbe wa bodi hiyo iliyojikita katika elimu ya michezo kwa watu wenye ulemavu wa akili Tanzania.