Polisi watamba kutwaa ubingwa michuano ya Netiboli

Kocha wa timu ya Polisi Arusha (katikati) Merenciana Silas akipokea msaada wa jezi za kuchezea kutoka kwa mkurugenzi wa kampuni ya usafirishaji ya Coast Liner,  Zouhra Ally ( mwenye nguo nyeusi) katika kuwasapoti kushiriki vema michuano ya ligi daraja la kwanza kwa mchezo wa netiboli inayotarajiwa kuanza June 20 hadi 29 jijini Dar-es-salaam wengine ni Baadhi ya wachezaji wa timu ya Polisi Arusha

Muktasari:

  • Michuano wa ligi daraja la kwanza kwa mchezo wa netbali inatarajia kuanza kutimua vumbi june 21 hadi 29 mwaka huu jijini Dar-es-salaam.

Kikosi cha timu ya Polisi Arusha kimeanza tambo za mapema za kunyakua ubingwa wa michuano wa ligi daraja la kwanza kwa mchezo wa netbali inayotarajia kuanza kutimua vumbi june 21 hadi 29 mwaka huu jijini Dar-es-salaam.


Timu ya polisi ambayo ndio pekee inayowakilisha mkoa wa Arusha katika mashindano hayo ya kitaifa, imetoa tambo hizo baada ya kupokea msaada wa vifaa vya michezo kutoka kampuni ya usafirishaji ya 'Coast Liner'.


Kocha wa Timu ya Netiboli ya Polisi Arusha, Emerenciana Silas alisema kuwa mwaka huu wamejipanga vema kuhakikisha hawapotezi alama katika michuano hiyo ya ligi daraja la kwanza itakayowasadia kutwaa kikombe cha klabu bingwa.


"Tunashukuru kampuni ya usafirishaji ya 'Coast Liner' kwa sapoti hii hasa jezi na tunawaahidi hatutawaangusha kwani tuko tiyari kwa ligi ya Netiboli na  tumefanya mazoezi zaidi ya mwezi mzima hapa katika viwanja vya Sheikh amri Abeid, lengo ni kuhakikisha kila mechi kwetu ni muhimu kuvuna alama" alisema Silas

Alisema kuwa kikosi chake kinajumuisha jumla ya wachezaji 11 ambao wote watasafiri hadi Dar-es-salaam kuhakikisha wanatekeleza maelekezo waliyoyapata katika mazoezi itakayofanikisha kutimiza malengo yao msimu huu.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi ya Coast Liner, Zohra Ally alisema kampuni yake imekuwa ikisapoti shughuli za michezo nchini ili kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu lakini pia kurudisha shukrani kwa jamii wanaofanikisha kampuni yao kufanya kazi nchini.

Alisema kwa upande wa mchezo wa Netiboli ndio wameanza kutoa misaada hiyo ikiwemo jezi na imedhamiria kuendelea kugawa katika michezo mingine pia.

"Coast Liner tunapenda kurudisha fadhila kwa jamii, kwa hiyo timu ya netiboli ya Polisi Arusha ilipoomba msaada wetu tuliitikia kwa kutoa vifaa kamili vya michezo kwa timu ya Mkoa ili kuwaongezea deni la kwenda kufanya vizuri kwenye mashindano haya ya klabu bingwa," aliongeza Zohra Ally.

Kamishna Msaidizi wa Polisi, Salvas Makweli aliyepokea msaada huo, mbali na kushukuru lakini pia alitumia fursa hiyo kuomba makampuni mengine na wanajamii kuendelea kuisaidia timu hiyo ya netiboli ambayo sasa inawakilisha mkoa wa Arusha.