Polisi Tanzania yaikamia Transit Camp

Muktasari:

Timu ya Polisi Tanzania imeapa kupata ushindi katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza unaotarajiwa kuchezwa Jumapili wiki hii kwenye Uwanja wa Chuo cha Ushirika, Moshi.

Kocha wa Polisi Tanzania Issah Rugaza, alisema ana matumaini ya kupata ushindi katika mchezo huo ili kurejesha matumaini baada ya timu hiyo kufungwa bao 1-0 na Geita Gold Mine katika mchezo uliopita.

Arusha. Timu ya Polisi Tanzania imeapa kuutumia vema uwanja wake wa nyumbani wa Ushirika Moshi kujiongezea pointi tatu muhimu itakapoikaribisha Transit Camp ya Dar es Salaam katika mechi ya Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.

 kocha wa Polisi Tanzania, Issah Rugaza alisema baada ya kupoteza mchezo uliopita kwa kufungwa 1-0 na Geita Gold kwenye Uwanja wa Nyankumbo mkoani Geita, wamepania kusawazisha makosa.

Alisema Polisi Tanzania iliumizwa na matokeo hayo hivyo itautumia mchezo huo kufikisha ujumbe kwa mashabiki wake kuwa iliteleza na sio kushuka kiwango.

Rugaza alisema kuwa katika mchezo huo wataingia uwanjani kwa tahadhari kwani wanafahamu Transit Camp ni timu inayoundwa na wachezaji mahiri na inao uzoefu wa kutosha.

“Mechi iliyopita tulifungwa 1-0 na Geita Gold ugenini matokeo yale yalituumiza sana lakini kwa kuwa bado mapema hasira zetu tutaingia nazo uwanjani siku ya Jumamosi ‘kesho’ kuhakikisha tunaishinda Transit Camp” alisema Rugaza.

Alisema hawatabweteka bali watacheza kwa kujituma kama vile wako ugenini ili kuhakikisha wanatimiza malengo yao ya kuondoka uwanjani na pointi tatu.

Kocha huyo alisema kuwa wameanza kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi kila siku kwa ajili ya kuwafanya wachezaji kuuzoea kwani ndio waliochagua kuwa Uwanja wao wa nyumbani.

Aidha alisema amezungumza na wachezaji wake na kuwataka kujituma katika mechi zote zilizo mbele yao kuhakikisha hawaruhusu kufungwa bao na huku wao wakiitumia kila nafasi watakayoitengeneza.