Pointi tatu tata Dabi ya Kariakoo

Muktasari:

  • Huu ni mchezo wa pili wa Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya timu hizo kukutana kwenye mchezo wa kwanza mwaka jana na Simba ikalala kwa mabao 5-1, kwenye uwanja huohuo wa Mkapa.

Simba itakuwa mgeni wa Yanga kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara Jumamosi ijayo, mechi ambayo itakuwa na maswali mengi ambayo yanahitaji majibu.

Huu ni mchezo wa pili wa Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya timu hizo kukutana kwenye mchezo wa kwanza mwaka jana na Simba ikalala kwa mabao 5-1, kwenye uwanja huohuo wa Mkapa.

Simba inakwenda kwenye mchezo huu ikiwa haijashinda michezo minne mfululizo ya michuano yote, ililala kwa bao 1-0 dhidi ya Al Ahly kwenye Uwanja wa Mkapa, ikachapwa 2-0 kwenye Uwanja wa Cairo International, ikapigwa kwa penalti 6-5 na Mashujaa ya Kigoma, kabla haijatoka sare ya bao 1-1, ilipovaana na Ihefu.

Lakini inakutana na Yanga ambayo nayo haipo vizuri sana kwenye michezo minne iliyopita, imeshinda miwili na kupoteza mmoja kwa penalti na sare mmoja.

Yanga ilitoka sare ya 0-0 na Mamelodi kwenye Uwanja wa Mkapa, ikafungwa kwa penalti 3-2 nchini Afrika Kusini baada ya suluhu dakika tisini, pia akaichapa Dodoma Jiji 2-0 na kumaliza dhidi ya Singida Foutain Gate kwa kushinda 3-0.

POINTI TATU ZENYE MAANA TATA

Timu zote mbili zinaingia kwenye mchezo huu zikiwa zinatafuta pointi tatu muhimu za ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Pointi ya tatu kwenye mchezo huu zina maana tofauti kwa timu zote mbili, Simba endapo itaambulia ushindi hapa itakuwa imerudi rasmi kwenye vita ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Lakini endapo Yanga itapata ushindi itakuwa imejiweka kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo kwa kuwa inaonekana itakuwa haina mpinzani aliyepo karibu yake.

Iko hivi, kwa sasa Yanga imekusanya pointi 55 baada ya kucheza michezo 21 ya Ligi Kuu msimu huu, Simba ipo nafasi ya tatu na pointi 46 ikiwa mchezo mmoja pungufu dhidi ya Yanga, baada ya yenyewe kucheza michezo 20.

Tofauti ya pointi za Yanga na Simba ni tisa, hivyo kama Yanga ikipata ushindi itakuwa imefikisha pointi 58 ambazo zitakuwa 12 mbele ya Simba ambayo kama ikishinda kiporo chake itazipunguza hadi tisa, yaani michezo mitatu.

Kwa upande wa Simba endapo ikishinda mchezo huu itafikisha pointi 49, maana yake tofauti yake na Yanga itakuwa pointi sita, endapo itashinda mchezo wake wa kiporo zitakuwa zimebaki tatu na hivyo mbio za ubingwa zitakuwa zinaanza rasmi.

Hii inaonyesha kuwa kila timu inakwenda kwenye mchezo huu ikiwa na mawazo tofauti na ndiyo mchezo ambao umeshikiliwa ubingwa wa ligi hiyo msimu huu, zikiwa zimebaki wastani wa mechi nane ambazo zina jumla ya pointi 24.

Lakini endapo Yanga ikishinda tofauti ya pointi 12 zitakuwa nyingi jambo ambalo litaifanya Simba isubiri Yanga ipoteze nusu ya michezo iliyobaki kwenye ligi ili iweze kutwaa ubingwa msimu huu jambo amba-lo linaonekana kuwa gumu kwa kuwa timu hiyo kwenye michezo 22 imepoteza miwili tu.

AZAM INAISHANGILIA YANGA?

 Matokeo ya mchezo huu yana maana kubwa kwa Azam pia ambayo ipo nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na pointi 50 zikiwa ni tano nyuma ya Yanga.

Mambo mawili yanaweza kutokea kwenye mchezo huu, endapo Yanga itaibuka na ushindi kwenye mechi hii itakuwa imeisaidia pia Azam kuendelea kuwa na uhakika wa kumaliza nafasi ya pili au kuwania ubingwa hivyo kuanza kujiandaa na kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Simba inaweza kuanza kufikiri kuhusu Kombe la Shirikisho Afrika.

Endapo Simba itashinda kiporo chake dhidi ya Azam itafikisha pointi 49 moja nyuma ya Azam, hivyo ili Simba imalize nafasi ya pili italazimika pia kuibuka na ushindi kwenye mchezo wake dhidi ya Azam baadaye ndiyo njia pekee ambayo inaweza kuwapa nafasi ya kuwa na matumaini ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

LIGI INAIBEBA YANGA

Msimu huu wa ligi umekuwa upande wa Yanga zaidi ikiwa imepoteza pointi nane tu, ikiwa imefungwa michezo miwili yenye pointi sita, lakini ikatoka sare michezo miwili hivyo ikiwa ndiyo timu ambayo imepoteza pointi chache msimu huu kwenye ligi hadi sasa.

Lakini kwa upande wa Simba mambo kwao yamekuwa tofauti wakati wanaelekea kwenye mchezo wa Dabi ya Kariakoo ikiwa imepoteza pointi 14 hadi sasa.

Imepoteza michezo miwili sawa na Yanga yenye pointi sita, lakini mbaya zaidi imetoka sare kwenye michezo minne hivyo kupoteza pointi nane kwenye sare hizo, bado pengo hili linaweza kuzibwa endapo tu Simba itafanikiwa kuibuka na ushindi hapa kwa Mkapa Jumamosi, matokeo mengine yoyote yatakuwa na faida zaidi kwa Yanga.

Suala la kufunga mabao, Yanga ambayo ililingana na Simba kwenye Ligi ya Mabingwa hatua ya makundi kwa kila moja kufunga mabao tisa, kwenye ligi imeonekana kuwa tofauti sana na wapinzani wao hao ikiwa imefunga mabao 52 kwenye michezo 21, ukiwa ni wastani wa zaidi ya mabao mawili kwenye kila mchezo.

Lakini Simba ipo nyuma ya Yanga pamoja na Azam ikiwa imefunga mabao 40 yakiwa ni 12 nyuma ya Yanga lakini saba nyuma ya timu inayoshika nafasi ya pili Azam.

Hivyo moja ya eneo lingine ambalo Simba inatakiwa kuwa nalo makini zaidi kwenye mchezo huu ni hili, kwani safu yake ya ulinzi imeonekana kutokuwa makini kwenye michezo minne iliyopita ikiwa imeru-husu mabao matano ndani ya dakika tisini, lakini Yanga haijaruhusu bao lolote kwenye idadi hiyo ya michezo ndani ya dakika tisini.

Picha hii inaonyesha pia uhalisia kwenye Ligi Kuu Bara ambapo Yanga ndiyo timu ambayo imefungwa mabao machache zaidi hadi sasa ikiwa nyavu zake zimetikiswa mara 11 tu kwenye michezo 21, lakini Simba imefungwa mabao 19 yakiwa ni nane mbele ya Yanga.

Simba kwa msimu huu ndiyo timu inayotengeneza nafasi nyingi zaidi lakini inashindwa kuzitumia hata kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo ilikuwa na timu kubwa kadhaa zikiwemo Mame-lodi na Al Ahly bado Simba ilionekana kuwa bora zaidi yao kwenye kutengeneza nafasi nyingi za mabao lakini ikashindwa kuzitumia.

Kwenye michuano hiyo Simba ilitengeneza nafasi 19 jumla, lakini ikafunga mabao tisa tu, ikiwa imepoteza nafasi kumi kuonyesha kuwa inatatizo kubwa kwenye eneo la ufungaji pekee, wakati Yanga ilitengeneza nafasi 13 tu na kufunga mabao tisa, hivyo nne tu ndiyo zilipotea.

Lakini kwenye eneo la kupiga pasi za uhakika Simba ipo juu ya Yanga ikiwa ina wastani wa pasi  329.9 kwa mchezo mmoja tofauti na Yanga ambayo wastani wake wa pasi kwenye mchezo mmoja ni 316.5 ndani ya dakika tisini jambo ambalo mashabiki wanatakiwa kulitarajia zaidi kwenye mchezo huu.

MAONI YA MAKOCHA

Charles Mkwasa ambaye aliwahi kuichezea Yanga na kuiongoza akiwa Kocha Mkuu katika Kariakoo Dabi iliyochezwa Januari 04, 2020 na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2, amewapa angalizo Yanga kuelekea mchezo dhidi ya Simba.

“Ninawapa angalizo Yanga wanapoingia kwenye mchezo huo kucheza kwa kuheshimu kwa kuwa dabi haina mwenyewe. Ninaipa mechi hii 50 kwa 50, kwani haieleweki, timu zote ziingie kwenye mchezo huo kuonesha ufundi na sio kukamia, timu yoyote itakayokuwa vizuri kwa siku hiyo basi itaondoka na matokeo chanya,” alisema Mkwasa.

Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji, Francis Baraza amesema utakuwa mchezo mzuri na wa ushindani huku akikiri kwamba, vita itakuwa eneo la kiungo, akibainisha kuwa limekamilika kila upande.

“Simba ina wachezaji wengi wenye uzoefu na dabi, kihistoria timu iliyo bora ndio inapata shida kwenye mechi ya dabi kutokana na kuingia kwa kujiamini, hivyo mashabiki watarajie dakika 90 za ushindani, hautakuwa mpira wa kupasiana sana kama ilivyozoeleka kwenye mechi za kawaida.”