Pochi nene, klabu zilizotumia pesa kunasa mastaa Ligi Kuu England

LONDON, ENGLAND. BAADA ya dirisha la usajili kufungwa Oktoba, 5, baadhi ya timu za Ligi Kuu, England zimeonekana kutumia mkwanja mrefu kulipa ada za wachezaji zilizowahitaji katika kuboresha vikosi vyao.

Hata hivyo, baadhi zimefanya usajili dakika za mwisho kabla dirisha halijafungwa, huku nyingine zilifanya mwanzoni mwa dirisha na tayari wameshaonyesha umuhimu wao kwenye vikosi vyao tangu msimu uanze.

Moja ya sajili zilizoonyesha kiwango ni wa James Rodriguez aliyetua Everton akitokea Real madrid ya Hispania.

Hizi hapa timu tano zilizokamua mkwanja dirisha hili lililofungwa juzi tu na kunasa mastaa wao.

5. Manchester United

Pauni 87 milioni

Ilitumia Pauni 87 milioni kusajili kabla ya dirisha kufungwa na ilifanikiwa kuwapata Amad Diallo kwa Pauni 19 milioni, Alex Telles Pauni 18 milioni na Facundo Pellistri Pauni 10 milioni.

Usajili wa mapema ulikuwa wa Donny van de Beek kutoka Ajax akiwagharimu Pauni 40 milioni. Pia imewauza Alexis Sanchez ambaye mpaka sasa haijajulikana Inter Milan imelipa shilingi ngapi ili kumsainisha moja kwa moja.

Pia timu hiyo ilifanikiwa kumuuza mlinzi wa kati, Chris Smalling kwa ada ya Pauni 13 milioni.

4. Everton

Pauni 87 milioni

Imekuwa na mwendelezo wa kutumia pesa nyingi kwenye soko la usajili na matokeo chanya yameonekana kwa kuwa inafanya vizuri Ligi Kuu.

James Rodriguez ambaye ameonekana akisumbua sana alisajiliwa kwa Pauni 20 milioni tu huku kiasi kingine kikitumika kwenye usajili wa Ben Godfrey, Allan Marques na Abdoulaye Doucoure

3. Leeds United

Pauni 96.4 milioni

Ilimsajili Rodrigo Moreno ambaye alivunja rekodi ya usajili ya klabu hiyo kwa kuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa kwa pesa nyingi akinyakuliwa kwa dau la Pauni 28 milioni kutoka Valencia na alifunga katika mchezo dhidi ya Manchester City ambapo mchezo ulimalizika kwa sare.

Mbali ya Moreno Leeds iliwasajili Robin Koch na Diego Llorente ambaye alichukuliwa baada ya mchakato wa kuipata saini ya Ben White kutoka Brighton kukwama. Mwisho ilimnyakuwa Raphinha, kwa dau la Pauni 17 milioni kutoka Rennes, kiujumla ilitumia Pauni 96.4 milioni.

2. Manchester City

Pauni 138 milioni

Safu ya ulinzi ilionekana kuwa mbovu kwa msimu uliopita, hali iliyosababisha ipambane kufanya usajili wa wachezaji wa eneo hilo. Ilimsajili mchezaji wa zamani wa Chelsea aliyekuwa anaichezea Bournemouth, Nathan Ake iliyemsajili kwa dau la Euro 45 milioni pamoja na beki wa kati wa Benfica, Ruben Dias kwa dau la Euro 68 milioni. Pia iliachana na David Silva aliyejiunga na Real Sociedad akiwa mchezaji huru na winga Leroy Sane ambaye ilimuuza kwa Euro 45 milioni kwenda Bayern Munich.

1. Chelsea

Pauni 222 milioni

Ndio inashika namba moja kwenye kinyang’anyiro hichi, ikiwa imetumia Pauni 222 milioni kwa wachezaji watano, ukiacha Thiago Silva na Malang Sarr ambao iliwasajili wakiwa mchezaji huru, ilitumia mpunga huo kwenye usajili wa Kai Havertz, Ben Chilwell, Hakim Ziyech na Edouard Mendy. Pia imeingiza Pauni 50 milioni baada ya kumuuza Alvaro Morata kwenda Atletico Madrid.