Pluijm: Mziki ndio umeanza hivo

KOCHA Hans Van Pluijm wa Azam, ametamba kugawa dozi kwa michezo yake ijayo ikiwa ni kutimiza malengo ambayo wamejiwekea msimu huu.
Azam imeanza Ligi kwa kishindo baada ya kushinda mechi zake mbili mfululizo, imeshinda 2-0 dhidi ya Mbeya City, 3-0 dhidi ya Ndanda FC katika michezo yao yote waliyocheza kwenye uwanja wao wa nyumbani, Azam Complex.
Akizungumza na Mwanaspoti, Pluijm alisema ushindi mfululizo umeongeza morali katika kikosi chake, lakini hilo linatokana na namna ambavyo wachezaji wanafuata maelekezo yake kwa umakini.
“Siri kubwa ya ushindi ni kujituma katika mazoezi yetu ya kila siku, pia tuna malengo ambayo tumejiwekea sisi kama timu kwahiyo tupo katika kutimiza malengo hayo kwa kila mchezo unaokuja mbele yetu,” alisema.
Akizungumzia kuhusu mifumo ambayo atakuwa anaitumia, alisema hawezi kubadilisha mfumo wake popote anapokwenda kwasababu hiyo ndio mbinu ya kumpa ushindi.
“Mifumo sio mara zote kwamba ndio huwa inafanya timu ishinde, kikubwa watu wanabidi waelewe kwamba sitoacha kutumia aina ya ufundishaji wangu ambao umezoeleka siku zote, naweza nikawa na mfumo mzuri lakini ufundishaji mbovu ndio maana nasema sitoacha aina ya soka langu” alisema.
Pluijm ambaye anasifika kwa soka lake la chini na kuhitaji matokeo katika kila mchezo, huku sehemu yoyote anayoenda huwa anapenda kutumia wachezaji wazoefu kupata matokeo kama ilivyokuwa Yanga akiwa na Amis Tambwe na wengine, Singida akiwa na Shafik Batambuze beki aliyekuwa na msaada katika kikosi hicho na sasa Azam, ambapo amefanya usajili wa wachezaji katika nafasi muhimu kwa kumrejesha Donald Ngoma na Danny Lyanga ili kuimarisha safu ya ushambuliaji.