Pluijm asajili Singida Utd

Muktasari:
- Tayari ameshuhudia usajili wa kiungo Tafadzwa Kutinyu aliyekuwa anaichezea Chicken Inn inayoshiriki Ligi Kuu Zimbabwe
SINGIDA United huenda ikamtangaza kocha wa zamani wa Yanga, Mholanzi Hans Pluijm, kuwa mkuu wa benchi lake la ufundi huku pia ikielezwa kwamba tayari kocha huyo ameanza mchakato wa kupitia mafaili ya wachezaji wapya ambapo kuna mapendekezo ya nyota watano wa kigeni kutoka Zimbabwe na Rwanda.
Tayari ameshuhudia usajili wa kiungo Tafadzwa Kutinyu aliyekuwa anaichezea Chicken Inn inayoshiriki Ligi Kuu Zimbabwe aliyesaini mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo ipo kwenye hatua za mwisho kukamilisha usajili wa straika Simbarashe Nhivi, beki wa kati Elisha Muroiwa pamoja na mshambuliaji kutoka timu ya Polisi Rwanda, Danny Usengimana.
Akiwa Yanga kabla ya kubadilishiwa majukumu kuwa Mkurugenzi wa Ufundi, Pluijm alimsajili straika Donald Ngoma kutoka Platnum ya Zimbabwe pamoja na Thaban Kamusoko na bado ameelekeza jicho lake huko huko.
Habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam, zinaeleza kwamba mdau mkubwa wa timu hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba ndiye anafanikisha kwa asilimia kubwa kukamilisha mambo ya usajili pamoja na suala la kocha Pluijm.
Mwanaspoti lilimtafuta Katibu Mkuu wa Singida United, Abdulrahiman Sima, ili kutoa ufafanuzi juu ya masuala hayo mawili na alisema: “Kuhusu usajili tumemsainisha mkataba wa miaka miwili Kutinyu na tupo kwenye mazungumzo na wachezaji wengine watatu wa kigeni, tukimalizana nao tutawatangaza.
“Kuhusu kocha Pluijm siwezi kulizungumzia hilo kwa sasa, muda ukifika itajulikana tu wala hakutakuwa na kificho, kama mpango upo basi utakuwepo kama haupo basi tutajuw, maana huwezi kuzungumzia kitu ambacho pengine kisiwe na ukweli.”
Alisema safu watakazoziimarisha kwenye kikosi chao ni kipa, washambuliaji wawili, beki wa kati wote kutoka nje ya nchi na watakaokuwa wanazochezea timu zao za taifa.