Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pina mwamba aliyeandika rekodi mpya Zanzibar

Muktasari:

  • Pina aliyekosa mechi saba kati ya 27 ilizocheza timu hiyo anamiliki mabao 19, amekuwa gumzo kwa kufunga hat trick mbili katika mechi moja ya ligi shidi ya Tekeleza walipoifumua 11-1 akifunga saba peke yake.

UNGUJA: STRAIKA wa Mlandege na nyota wa timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, Abdallah Idd ‘Pina’ ameweka rekodi Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) wakati msimu ukiwa ukingoni.

Pina aliyekosa mechi saba kati ya 27 ilizocheza timu hiyo anamiliki mabao 19, amekuwa gumzo kwa kufunga hat trick mbili katika mechi moja ya ligi shidi ya Tekeleza walipoifumua 11-1 akifunga saba peke yake.

Mabao hayo yamemfanya Pina kuwa mchezaji pekee msimu huu kufanya hivyo, huku mwenyewe akiweba bayana kiu yake ni kutaka kuvunja rekodi ya Suleiman Mwalimu ‘Gomez, nyota wa zamani wa KVZ anayekipiga Wydad Casablanca nchini Morocco.

Straika huyo aliyeianza safari ya soka 2015, kwa sasa akitimiza miaka 10 ya kupambania ndoto amezichezea timu mbalimbali ndani na nje ya Zanzibar.

Akizungumza na Mwanaspoti katika mahojiano maalumu nyumbani Mchina mjini hapa, anasema anafurahishwa na safari hiyo kwa kuwa ni kijana mdogo anayefanya vizuri katika soka la Zanzibar.

Nyota huyo amewahi kuzichezea Magomeni(2015), Gulioni (2015), Jang’ombe Boys (2016), Polisi Tanzania (2020), Kipanga (2021), Kundemba(2023) na Mlandege kwa ndani.

Nje ya Tanzania aliwahi kucheza katika ligi ya mafuta Alzakhir Dubai 2017, timu ya Chaux Sport (2023) iliyopo Kongo na alitakiwa Vipers nchini Uganda, lakini walishindwana katika mazungumzo.

Akiulezea mchezo wa Tekeleza ambao ulisababisha rikodi ya kufunga mabao mengi, anasema alijisikia amani kupata ushindi kwani ni mtu pekee aliyefunga mabao mengi katika mchezo mmoja msimu huu.

Pina anasema licha ya kuwa Mlandege ilitaka kushinda dhidi ya timu hiyo, upande wake alikuwa na lengo la kufunga mabao mengi ili kuweka historia nzuri ya msimu na kubeba kiatu cha ufungaji.

Mshambuliaji huyo anasema siri ya kufunga mabao mengi katika mchezo huo ni kwa kuwa aliona udhaifu wa wapinzani wao kuwa na kwamba hawakutaka matokeo mazuri, hivyo wao ndio walioonyesha hamu ya kutoka na matokeo mazuri, jambo lililomfanya kuongeza ari na bidii kutafuta mabao.

Anaongeza kuwa, licha ya Tekeleza kutohitaji matokeo mazuri, lakini ilikuwa na jitihada nzuri za kucheza kwa utulivu bila hofu ndipo walipotumia kila nafasi ambayo waliipata kutafuta bao na kutoka na matokeo mazuri.

Anasema alikuwa na jitihada katika mchezo huo tofauti na wachezaji wengine waliokuwepo kuhakikisha kuwa lengo linatimia.

“Katika mchezo huo nilikuwa nafunga na wakati huohuo nilikuwa natengeneza nafasi kwa wengine kufunga mabao hadi nilipofunga saba... kila muda nilikuwa natabasamu peke yangu kutokana na furaha niliyoipata kwani juhudi zangu zimezaa matunda mazuri kwangu,” anasema Pina

Mshambuliaji huyo aliyecheza mechi 19 na kuvuna mabao 17, lakini saba aliyoifunga Tekeleza yamemuweka katika nafasi nzuri na kuandika historia msimu huu kuwa mchezaji pekee aliyefunga mabao mengi mchezo mmoja.

Pina amefanikiwa kuvunja rekodi ya Mwalimu kufunga mabao mengi katika mchezo mmoja.

Mwalimu alikuwa na rekodi ya kufunga mabao matano katika msimu mmoja uliopita dhidi ya Maendeleo United ya Pemba ambapo Pina kaivunja. Kwa sasa Pina amebakisha mabao matatu ili kuifikia rekodi ya Mwalimu aliyefunga mabao 20 msimu uliopita na kuibuka mfungaji bora wa ligi hiyo.

Hata hivyo, Pina anasema nguvu na jitihada anazotumia kuongeza mabao ni kwa sababu anahitaji kuwa mfungaji bora msimu huu, huku ikibaki michezo mitano msimu kumalizika.

Sambamba na hayo, mshambuliaji huyo anasema mpira ni kipaji cha urithi kutoka kwa baba yake ndio maana hatumii nguvu nyingi badala yake anatumia uwezo na mafunzo anayopewa kuongeza ufanisi.


UHUSIANO NA TIMU

Mshambuliaji huyo anasema Mlandege inamfanya kuishi bila mawazo kutokana na imani kubwa aliyoijenga kupitia viongozi hadi wachezaji wenzake.

Pina anasema uwepo wake katika timu hiyo imekuwa furaha kwake, mashabiki na wachezaji wezake.


CHANGAMOTO, USHAURI

Mshambuliaji huyo anasema kupitia soka amepata mafanikio, lakini anakabiliwa na changamoto ya baadhi mabeki wa Ligi Kuu kuwa na maelekezo yanayohusiana na yeye jambo ambalo anahisi litampotezea kipaji ambacho ndio ajira kwake.

Anadai baadhi ya makocha wanaofundisha mpira katika baadhi ya timu wanachukua vipande vya picha jongefu kufundishia dhidi ya Mlandege.

“Baadhi ya makocha wanatumia video zangu kufundishia ili nisiweze kupata bao katika mechi kwani wanasoma mbinu ambazo natumia na sipendi hilo,” anasema Pina. Hata hivyo, hilo ni jambo la kawaida kwa makocha kutumia video kufundishia soka dhidi ya timu wanazokabiliana nazo.

Pia anadai mabeki  huanza kutiwa sumu na viongozi wao dhidi yake na hata anapoendelea kufunga baadhi ya wachezaji na viongozi wanafanya mbinu kukosa mabao akiwa katika mchezo.

Anadai wakati mwingine mabeki wa timu pinzani humchezea rafu na kumuumiza jambo ambalo si jema kwa sababu wote ni watafutaji.

Mbali na hayo, Pina anatoa wito kwa washambualiaji chipukizi wanaotamani kuwa kama yeye kujitunza kwa kujiepuka na vishawishi ikiwemo kutumia dawa za kulevya, pombe na kuendekeza ngono kupita kiasi.

Pia, anawataka wachezaji  chipukizi kuwa na jitihada ikiwemo kufanya mazoezi binafsi na kujituma kwani hiyo ndio njia pekee ya kuyafikia mafanikio.

Nje na soka, mchezaji huyo anasema hufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kuuza duka la vifaa vya magari, biashara ya usafirisha kwa kutumia  bajaji na pikipiki ili kujiongezea kipato.

Pina anasema katika maisha ya kawaida hapendi kujichanganya sana na watu ambao si wazuri kwani anapendelea zaidi kujulikana kwa mazuri na si mabaya ambayo yatamfanya kudharaulika katika jamii.

Vilevile, anasema siku ambazo haendi dukani anapotoka mazoezini hupendelea zaidi kutulia nyumbani kwani jambo hilo linamsaidia kuufanya mwili kuwa imara.

Anasema mtu pekee ambaye anamhamasisha katika soka ni baba yake na ndiye mshauri wake mkubwa. Nyota huyo anasema hakuna mchezaji mwingine kitaifa wala kimataifa anayetamani kuwa kama yeye.

Anasema anaamini Cristiano Ronaldo na Lionel Messi waliamini vipaji ndio maana wamefika walipostahili hivyo naye anaishi katika ndoto hizo.

Mshambuliaji huyo anasema anatamani kucheza nje ya Zanzibar ili watu wajue uwezo aliobarikiwa na Mungu na anazikaribisha timu ambazo zinamtaka kufanya mazungumzo na Mlandege.