Phiri ataka mataji Msimbazi

MSHAMBULIAJI mpya wa klabu ya Simba Moses Phiri raia wa Zambia aliyekuwa akikipiga timu ya Zanaco, amekiri ujio wake umechagizwa na mastaa wa klabu hiyo Rally Bwalya na Clatous Chama.

Phiri ametambulishwa rasmi jana kuwa staa namba moja katika usajili, baada ya dili lake kukamilika toka mwaka jana, wakati huo watani zao Yanga wakimkosa.

Akizungumza baada ya kuwasili Msimbazi Phiri alisema, amekuja sehemu sahihi ya ndoto yake  kutokana na ukubwa wa klabu hiyo katika ukanda huu wa Afrika.

"Nimefuatwa pia na timu nyingine hapa Tanzania, lakini ubora wa Simba ndio ulionifanya nije kutimiza  ndoto yangu, na malengo yangu ni kusaidia timu kurudi katika njia yake ya kutwaa mataji msimu ujao," amesema Phiri.

Aidha Phiri amesema, alikuwa akitamani kucheza soka la Tanzania kutokana na marafiki zake Bwalya na Chama wanavyoishi hivyo hana wasiwasi katika jambo la kuwapa furaha mashabiki wa msimbazi kwa kuwa hilo ni jukumu lake.

Amesema kwa kushirikiana na wachezaji wenzake anaamini Simba msimu ujao itafikia malengo kuanzia ndani ya ligi na michuano ya Kimataifa ili kutinga nusu fainali.