Phiri aendeleza moto Ligi Kuu

Kipindi cha kwanza kimemalizika katika mchezo wa Ligi Kuu Bara Simba wenyeji wakiongoza mabao 2-0, dhidi ya Dodoma Jiji.

Katika mchezo huo mabao ya Simba yalifungwa na beki wa kati wa Dodoma, Abdallah Shaibu ‘Ninja’  aliyejifunga dakika 6, kabla ya straika hatari wa Simba kwa sasa, Moses Phiri kuweka kambani bao la pili dakika 45.

Phiri aliyesajiliwa na Simba msimu huu amekuwa mchezaji hatari kwenye kikosi hicho kutokana na kazi yake ya ufungaji mabao katika Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mechi tano za ligi Simba iliyocheza Phiri amefunga mabao manne katika michezo minne kasoro mmoja tu ule wa Tanzania Prison ambao bao la Simba lilifungwa na Jonas Mkude dakika za jioni.

Makali ya Phiri hadi katika Ligi ya mabingwa kwani kwenye michezo miwili iliyocheza Simba dhidi ya Nyasa Big Bullets Mzambia huyo amefunga yote.

Katika mchezo huu Simba ilionekana kutawala mechi haswa eneo la katikati mwa uwanja wakipigiana pasi ndefu na fupi tofauti na wapinzani wao Dodoma Jiji.

Kutawala huko mpira kwa Simba kuliwafanya kutengeneza nafasi za kufunga mabao zaidi ya hizo mbili walizotumia vizuri kwa kupata mabao.

Dodoma Jiji wao walikuwa na makosa ya kiulinzi na ukabaji haswa eneo lao la mabeki na hilo lilitokana na presha ya Simba kukaba kuanzia juu.

Katika eneo lankiungo Dodom Jiji walikuwa wakifanya kazi kubwa ya kukaba kuliko kucheza mpira na kuanzisha mashambulizi.

Dodoma mashambulizi yao yalikuwa ya kushtukiza na alimtumia zaidi, Collins Opare ambaye kuna nyakati alijaribu kuleta hatari langoni mwa Simba.

Opare muda mwingi alijikuta yupo chini ya ulinzi wa mabeki wa kati, Joash Onyango na Kennedy Juma waliokuwa makini kwenye kumzuia.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Simba ilikuwa mbele kwa mabao 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji.