Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Petit Sory aliupiga mwingi Guinea bongo ikazaa kituko

Muktasari:

Wakati Hafia FC ilitumia jezi nyeusi na nyeupe ilipoingia uwanjani kucheza dhidi ya Yanga, mwamuzi wa mchezo huo, Gratian Matovu, aliyesaidiwa na washika vibendera Manyoto Ndimbo na Kaabuka (wote marehemu) alionekana kuwa na kigugumizi cha kuanza mchezo.

MIONGONI mwa nchi za Afrika ambazo kiwango chake cha mchezo wa kandanda kimeanguka katika miaka ya karibuni ni Guinea.

Nilipoandika habari za michezo mwishoni mwa miaka ya 1960 hadi katikati ya miaka ya 1980 hapa nchini na nje kama mwandishi na baadaye Mhariri wa Michezo wa Daily News yapo mambo sitayasahau juu ya timu ya Guinea na klabu yake maarufu ya Hafia FC.

Lipo tukio moja la zama zile kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, katika mwaka 1972 ambalo kila nikilikumbuka hubaki ninacheka.

Wakati ule nikiwa Arusha kama mwandishi wa Daily News niliitwa Dar es Salaam ili kuandika habari za mechi za kirafiki kati ya timu ya Hafia FC ya Guinea iliyokuja nchini kwa mechi za kirafiki dhidi ya Yanga na Simba.

Siku zile, Hafia FC iliyokuwa iking’ara Afrika, ilikuwa inafika mara kwa mara Tanzania kwa michezo ya kirafiki na wakati wa sherehe za kitaifa.

Hii ilitokana na maelewano mazuri yaliyokuwapo kati ya Tanzania na Guinea na hasa kati ya marais wa nchi hizi mbili, Ahmed Sekou Toure na Mwalimu Julius Nyerere.

Wakati Hafia FC ilitumia jezi nyeusi na nyeupe ilipoingia uwanjani kucheza dhidi ya Yanga, mwamuzi wa mchezo huo, Gratian Matovu, aliyesaidiwa na washika vibendera Manyoto Ndimbo na Kaabuka (wote marehemu) alionekana kuwa na kigugumizi cha kuanza mchezo.

Niliwauliza waandishi wa habari wenzangu na wapiga picha (tulikuwa kama sita wakati ule) tuliokuwa pembezoni mwa uwanja nini kilitokea na wote walikuwa hawajui kama mimi.

Huku mashabiki waliojaza uwanja wakipiga kelele kutaka mchezo uanze, Matovu alikuja pembezoni mwa uwanja na kwenda kwenye benchi walipokaa viongozi na wachezaji wa akiba wa Hafia.

Kilichotamkwa na Matovu kilitushangaza na kucheka. Alimuuliza kocha wa Hafia (simkumbuki jina lake, lakini alikuwa raia wa Brazil na ambaye pia alikuwa kocha wa timu ya taifa ya Guinea) mbona alikuwa hamuoni Petit Sory (jina lake hasa ni Ibrahim Sory Keita).

Mchezaji huyu alifuatana na kikosi hicho katika ziara ile, lakini hakuingia uwanjani wakati ule.

Kocha alimwambia Matovu apulize filimbi ya kuanza mpira na angemuona uwanjani Petit Sory baadaye. Wakati ule wachezaji walipoingia uwanjani Petit alikuwa anasali katika chumba cha kuvalia wachezaji.

Aliingia uwanjani muda kidogo baada ya mchezo kuanza na kufurahisha watazamaji kwa mchezo maridadi na wa kuvutia.

Siku chache baadaye nilipomuliza Matovu kwa nini alifanya vile kwa kuwa waamuzi hawategemewi kufanya vile aliniambia alimuona mara nyingi Petit alipocheza na alifurahia mchezo wake licha ya kuwa muamuzi wa mchezo au ameshika bendera hivyo alitamani kumuona uwanjani.

Petit alikuwa kivutio cha kikosi cha Hafia FC ambacho zama zile kilikuwa hakishikiki katika Bara la Afrika. Hali hii ilisababisha kuwepo timu nyingi za watoto nchini na nchi jirani zilizoitwa Hafia FC.

Timu hii ya Conakry, mji kuu wa Guinea, ambayo ilianzishwa 1965 ilikuwa klabu bingwa ya Afrika miaka ya 1972, 1975 na 1977. Vile vile ilishika nafasi ya pili katika kinyang’anyiro hiki 1976.

Hafia ni moja ya klabu za Bara la Afrika zilizopata mafanikio makubwa kama Al Ahly na Zamalek za Misri na Hearts of Oak na Asante Kotoko za Ghana, Enugu Rangers ya Nigeria na Canon Yaounde ya Cameroon.

Petit aliyekuwa mchezaji wa kiungo aliyevaa jezi nambari 6, alikuwa na ustadi wa kumpokonya mpinzani mpira na alipoutia mguuni alitembea kwa madaha kama yange yange na kuwafungulia njia wenzake kufunga mabao.

Akiwa mchezaji mfupi zaidi katika kikosi cha Hafia FC (futi 5 na inchi 5 1⁄2 ) alishirikiana vizuri na Ibrahim Kandia na Soulamage Cherif.

Katika mwaka 1972 alipokuwa aking’ara wengi walitarajia gazeti la Kifaransa la Michezo “France Football” lililosimamia kuchagua mchezaji bora wa kandanda wa Afrika lingemchagua, lakini lilimpa nafasi ya tatu.

Wachambuzi wa michezo na siasa hawakushangazwa na uamuzi ule kwa vile Wafaransa walikuwa hawaupendi utawala wa Rais Sekou Toure ambaye aliwafukuza Wafaransa baada ya nchi hiyo kupata uhuru.

Petit alianza kung’ara akiwa na miaka 23 wakati wa michezo ya Olimpiki ya 1968 akiwa na kikosi cha Guinea na aliendelea kuwa hivyo mpaka mwishoni mwa miaka ya 1970.

Siku hizi husikika mara chache akisikitika namna heshima ya Guinea ilivyoporomoka katika mashindano ya kimataifa.

Alikuwa akifika sana viwanjani kwa miaka mingi baada ya kustaafu lakini tangu mwaka 2018 huonekana mara moja baada ya kifo cha mchezaji rafiki yake wa karibu na aliyekuwa nahodha wa Guinea, Papa Camara aliyefariki akiwa na umri wa miaka 66.

Vile vile husikitishwa kuona Hafia iliyokuwa bingwa nchini Guinea kwa miaka tisa mfululizo, kutoka 1971 hadi 1979, imepoteza umahiri wake. Badala yake imefunikwa na AS Kalom na Horaya FC na vijana wengi wa leo Afrika hawaijui klabu ya Hafia.

Kila nikikutana na kuzungmza na wachezaji wa zamani wa Tanzania karibu wote humsifia Petit Sory.

“Akiwa na mpira ilikuwa hujui ataelekea upande gani na ukimvamia utakula chenga ya maudhi. Alijiamini, licha ya ufupi wake kama wewe,” aliniambia mchezaji maarufu wa zamani wa Yanga na timu ya taifa, Athumani Kilambo.

Siku hizi Guinea inao wachezaji wachache Ulaya ukilinganisha na zamani kutokana na hali ya mchezo katika nchi hii ya Afrika ya Magharibi kupwaya na kutawaliwa na Ghana, Ivory Coast, Nigeria na Cameoon.

Hata hivyo, kila panapoelezewa kandanda nchini Guinea jina la Petit Sory huibuka juu kama mmoja wa wachezaji stadi aliyeipa nchi hii heshima katika kandanda miaka iliyopita.

Sijui hali leo itakuwaje uwanjani na katika vyombo ya habari akitokea muamuzi kuulizia kwa nini mchezaji mmoja wa timu anazozichezesha hayupo uwanjani kama alivyofanya Matovu.

Kwa kweli mchezo wa kandanda una mengi, lakini mengine huyaoni mpaka uchunguze kwa darubini.