Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Penalti zaleta mshtuko Jangwani

Yanga walikosa pia nafasi ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame kwa mwaka jana ambapo waliondoshwa na Azam katika hatua ya robo fainali kwa mikwaju ya penalti

Muktasari:

  • Iko hivi. Yanga juzi Jumatano ilipoteza mchezo wa Ngao ya Hisani kwa Azam baada ya kufungwa penalti 4-1 baada ya sare ya mabao 2-2 katika dakika 90 za mchezo huo. Nyota wawili wa Yanga, Hassan Kessy na Haruna Niyonzima walikosa penalti.

BENCHI la ufundi la Yanga chini ya Kocha Hans Pluijm limepigwa na butwaa. Wanachama na mashabiki wa klabu hiyo wamebaki mdomo wazi kwa bumbuwazi lililowapata, huku viongozi wakishindwa kuamini kilichowakuta. Hakuna anayeamini kama klabu yao imefikia ilipo, kisha kwa kauli moja wakasema ‘jamani imetosha’.

Unajua ni nini? Mikwaju ya penalti ndio tatizo kuu. Wanayanga wametaharuki baada ya kubaini kuwa timu yao imekosa mataji manne makubwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kutokana na mapigo hayo na mikwaju ya penalti.

Yanga imejikuta ikikumbana na kadhia ya ajabu baada ya kukosa nafasi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Kagame, Kombe la Mapinduzi na juzi Ngao ya Hisani ambapo kote huko waliondolewa kutokana na kupiga penalti mbovu.

Iko hivi. Yanga juzi Jumatano ilipoteza mchezo wa Ngao ya Hisani kwa Azam baada ya kufungwa penalti 4-1 baada ya sare ya mabao 2-2 katika dakika 90 za mchezo huo. Nyota wawili wa Yanga, Hassan Kessy na Haruna Niyonzima walikosa penalti.

Kabla ya mchezo huo, mapema mwaka huu Yanga ilitolewa katika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi na URA ya Uganda kwa mikwaju ya penalti baada ya sare ya bao 1-1 katika dakika 90. Malimi Busungu na Geofrey Mwashiuya walikosa penalti kwa upande wa Yanga.

Yanga walikosa pia nafasi ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame kwa mwaka jana ambapo waliondoshwa na Azam katika hatua ya robo fainali kwa mikwaju ya penalti baada ya sare tasa ndani ya dakika 90. Kipa wa Azam, Aishi Manula alipangua penalti ya Haji Mwinyi katika mchezo huo.

Mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara walipoteza pia nafasi ya kufanya vizuri katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2014 baada ya kufungwa penalti 4-3 na Al Ahly ya Misri baada ya matokeo ya jumla ya nyumbani na ugenini kuwa bao 1-1. Mbuyu Twite, Said Bahanuzi na Oscar Joshua walikosa penalti katika mchezo huo.

MSIKIE TIGANA

Nyota za zamani wa Taifa Stars, Ali Tigana alisema tatizo la kukosa penalti linachagizwa na mazoezi hafifu ya upigaji huo, kwani wachezaji wanatakiwa kuwa na mafunzo ya kupiga penalti kila siku ili kujenga hali ya kujiamini.

“Ufungaji wa penalti unategemea zaidi mazoezi, lazima kuwepo na mazoezi ya mara kwa mara ya upigaji wa penalti ili wachezaji wapate hali ya kujiamini na kuweza kufunga kwa urahisi,” alisema.

“Nakumbuka wakati nacheza tulikuwa na mafunzo ya kupiga penalti kila siku baada ya mazoezi ya kawaida, kila mchezaji aliweza kupata uzoefu wa kutosha katika mazoezi hayo na hatukupata shida katika mechi,” aliongeza.

Kipa wa zamani wa Yanga, Peter Manyika alisema tatizo kubwa la penalti linatokana na mchezaji mwenyewe kuamini kuwa ameshafunga wakati ambapo bado hajapiga mkwaju wenyewe.

“Penalti ni sehemu ambayo inahitaji uzoefu na mchezaji anatakiwa awe amefanya mazoezi ya kutosha, isiwe tu amefanya wakati anaelekea katika mchezo husika, kocha ni lazima afahamu kuwa kuna wakati penalti zitahitajika kuamua mchezo,” alisema.

“Mchezaji anaweza kufunga penalti kama anaichukulia kwa uzito unaostahili, hatakiwi kuamini hata kidogo kuwa tayari amefunga wakati bado hata hajapiga, hapo lazima akose,” alifafanua.

KOCHA PLUIJM

Kocha Hans Pluijm na benchi lake la ufundi amekuwa akishangaa namna vijana wake wanavyomuangusha kwenye adhabu hiyo ya penalti, kwani huwa amewapa mbinu zote za kutupia kambani.

“Sijajua hii inatokana na nini, ila nadhani wakati mwingine ni presha na kukosa umakini. Hakuna namna,” alisema Pluijm huku akisema katika pambano lao la juzi hawakustahili kufikishana hatua hiyo na Azam kwani walishamaliza kazi mapema.

“Umakini mdogo na kujisahau kwa vijana ndiko kulikotuponza, ila tunaangalia yaliyopo mbele yetu,” alisema Kocha huyo kutoka Uholanzi.