Prime
Pedro afunguka baada ya kutimuliwa Yanga
YANGA ilikuwa uwanjani jana usiku ikimalizana na Coastal Union katika mchezo wa kwanza tangu ilipomtimua kocha Pedro Goncalves, lakini mwenyewe ameibuka akitamba mambo manne huku akisema ameiacha timu hiyo ikiwa bingwa wa msimu huu.
Pedro aliyeiongoza Yanga kwenye mechi 19 za ligi bila kupoteza, ameliambia Mwanaspoti kwamba hana shida sana na maamuzi yaliyomshangaza ya kusitishiwa mkataba wake na kwamba ana furaha ya kuiacha timu hiyo ikiongoza msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi tano, wakati alipoikuta kulikuwa na tofauti ya alama mbili.
Pedro alisema kuwa furaha yake ni kwamba ameiachia Yanga Kombe la Mapinduzi, lakini mambo mawili yaliyomkosesha raha ni kushindwa kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika mchezo wa mwisho wa makundi, huku timu iliyowazuia kufuzu ikifika fainali.
Kocha huyo raia wa Ureno aliongeza kuwa jambo lingine lililomnyima raha ni kuukosa ubingwa wa Kombe la Muungano baada ya kupoteza dhidi ya Simba kwa bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali ulioenda dakika 120.
“Kwanza niseme, ukiacha taarifa ya kwenye Instagram, mpaka sasa sijapata taarifa kamili kutoka kwa uongozi. Nipo nasubiri, lakini naamini hii ni wikiendi, labda kuanzia Jumatatu watanitafuta na tutamalizana ili niendelee na mambo mengine,” alisema Pedro na kuongeza:
“Hapana, siwezi kuchukia. Nina amani kwa kuwa naiacha timu ikiwa salama. Wakati nafika hapa nilikuta kuna tofauti ya pointi mbili kati yetu na waliokuwa nafasi ya pili, na sasa naondoka wakati timu ina tofauti ya pointi tano.
“Usisahau Yanga ndiyo timu pekee hadi sasa ambayo haijapoteza mchezo wowote wa ligi. Kuna mengi sana tumepitia msimu huu, ikiwemo majeruhi wengi wa wachezaji muhimu, lakini bado hatukupoteza zaidi ya kutoa sare.
“Unazungumzia ushindi wa bao moja dhidi ya KMC, lakini jiulize Simba ilicheza vizuri dhidi ya JKT ambao sisi tuliwafunga mabao matano? Tulishinda bao moja dhidi ya KMC ambayo tuliifunga mabao mengi mzunguko wa kwanza.
“Mbona hamuulizi kwanini nilibadilisha sana kikosi kwenye mchezo dhidi ya KMC? Unawezaje kuwapa nafasi wale wale waliocheza mechi mbili ngumu dhidi ya Simba kwa jumla ya dakika 210? Nililazimika kubadilisha kikosi, lakini bado tulitawala mchezo na kutengeneza nafasi nyingi, ila wachezaji wakakosa utulivu wa kuzitumia. Katika mazingira kama hayo unamlaumu kocha?”
Kocha huyo alisema kuwa licha ya kuondoka ndani ya timu hiyo, anaamini kazi kubwa tayari ameifanya na kwamba Yanga tayari imebeba ubingwa wa ligi iwapo itashinda mechi nane zilizobaki.
“Mimi naondoka lakini naiacha Yanga ikiwa bingwa wa msimu huu. Kazi kubwa na ngumu, pamoja na nyakati ngumu na mechi nyingi ngumu, tayari zimeshapita. Huko ndiko kulikuwa kugumu kuliko mechi zilizobaki ambazo naamini zinawezekana kushinda,” alisema Pedro.