Pamba yafunga hesabu Nyamagana, yamwagiwa Sh10.5 milioni

Muktasari:

  • Ushindi huo unaifanya Pamba Jiji kufikisha pointi 61 na kuendelea kukamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa Championship, huku FGA Talents ikiwa katika nafasi ya 10 na alama zake 31.

Mwanza. PAMBA Jiji imehitimisha mechi za nyumbani msimu huu kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza kwa ushindi wa 1-0 na kuweka rekodi ya kutopoteza mchezo, huku kazi ikibaki jijini Arusha ambako hatma ya kupanda Ligi Kuu itaamuliwa.

Timu hiyo imepata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya FGA Talents ya Songea leo Aprili 13, 2024 kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza, bao pekee likifungwa na winga, Ismaily Ally katika dakika ya 16 kwa mpira wa kutengwa ambao ulijaa kambani.

Ushindi huo unaifanya Pamba Jiji kufikisha pointi 61 na kuendelea kukamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa Championship, huku FGA Talents ikiwa katika nafasi ya 10 na alama zake 31.

Ni mchezo wa mwisho nyumbani kwa Pamba msimu huu mbele ya mashabiki wao, ambapo inakwenda kumalizia mechi zake mbili za mwisho jijini Arusha Aprili 21 dhidi ya TMA kwenye Uwanja wa Black Rhino na Aprili 28 dhidi ya Mbuni kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Pamba inahitaji kushinda mechi hizo mbili ili kujihakikishia nafasi ya kupanda moja kwa moja kwenda Ligi Kuu Bara na kurudi jijini Mwanza ikiwa na shangwe kubwa kwa kutimiza ndoto ambayo imeshindikana kwa zaidi ya miaka 20.

Kwa maana hiyo, Pamba imefunga hesabu zake kibabe nyumbani ikimaliza kwa kuweka rekodi ya kutopoteza mchezo wa Ligi ya Championship kwenye Uwanja wa Nyamagana ambako imecheza mechi 14 ikishinda 11 na sare tatu dhidi ya Copco, Mbeya Kwanza na TMA, huku mchezo pekee iliopoteza nyumbani ilifungwa bao 1-0 na Biashara United ukichezwa Uwanja wa Mwadui, Shinyanga.

Baada ya ushindi huo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amewakabidhi wachezaji Sh10.4 milioni za motisha, kati ya hizo ofisi yake imetoa Sh5.2 milioni, huku akiahidi kuwajaza mamilioni zaidi katika michezo miwili ya mwisho ambayo itaamua hatma yao ya kwenda Ligi Kuu.

Kipa wa Pamba, Shaban Kado amefikisha 'clean-sheet' yake ya nane msimu huu akikamata nafasi ya nne nyuma ya Castor Mhagama wa Ken Gold mwenye 16, Yusuph Abudul wa TMA (15) na Robert Mapigano wa Biashara United (10).

Kocha Msaidizi wa Pamba, Renatus Shija amesema wachezaji wake hawakufanya vizuri leo kwani wameshindwa kutumia nafasi nyingi ambazo wametengeneza huku akidai watapaswa kubadilika katika michezo hiyo miwili ya mwisho ili wapate matokeo chanya.

Mjumbe wa bodi ya klabu hiyo, Evarist Hagila, amesema msimu huu wamedhamiria kuvunja mwiko wa kutopanda daraja huku akiwaahidi mashabiki kwamba uongozi umeweka nguvu ya kutosha katika michezo hiyo miwili.