Pamba yaanza hesabu za msimu ujao

Muktasari:
- Pamba Jiji licha ya kukamata nafasi ya 12 katika msimamo ikiwa na alama 30 baada ya mechi 28, ikishinda saba, sare tisa na kupoteza 12, ikifunga mabao 20 na kuruhusu 32, bado iko nafasi ya kucheza mechi za mtoano (play-offs) kuepuka kushuka daraja.
LICHA ya kubakiwa na mechi mbili tu kabla ya kuhitimisha msimu wa Ligi Kuu Bara wa 2024/2025, Pamba Jiji tayari imeanza kupiga hesabu za msimu ujao ikiwemo mustakabali wa mdhamini mkuu na maboresho ya kikosi chake.
Pamba Jiji licha ya kukamata nafasi ya 12 katika msimamo ikiwa na alama 30 baada ya mechi 28, ikishinda saba, sare tisa na kupoteza 12, ikifunga mabao 20 na kuruhusu 32, bado iko nafasi ya kucheza mechi za mtoano (play-offs) kuepuka kushuka daraja.
Mlezi wa timu hiyo, Said Mtanda akizungumza juzi jijini hapa baada ya kukutana na wadhamini wenza wa Pamba Jiji, Shirika la Bima la Taifa (NIC), aliwahakikishia timu haitoshuka daraja na tayari imeanza maandalizi ya kuboresha kikosi chao msimu ujao.
Mtanda ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza aliwashauri wadhamini hao kuongeza mkataba, kwani waliosaini wa mwaka mmoja umemalizika, huku akiwahimiza kupambana na kuongeza dau ili wapate nafasi ya kukaa kifuani katika jezi.
“Kuwekeza katika michezo ni vizuri na sio hasara tunawakaribisheni mfano GSM anapamba jezi ya Pamba, lakini kaweka Sh300 milioni tu, hivyo na nyinyi njooni na tunawahakikishia hatushuki daraja na msimu ujao tumepanga kuimarisha timu,†alisema Mtanda na kuongeza;
“Tumeshatoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Jiji kuzungumza na menejimenti ya NIC ili msimu ujao waendelee kuwa mtoa bima wetu lakini hii ni ‘toa kitu pata kitu’ lazima naye atuhakikishie kwamba atatusaidia na udhamini utakuwepo.â€
Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano shirika hilo la Bima, Karimu Meshack alithibitisha mkataba wa mwaka mmoja na klabu hiyo unamalizika, lakini wamevutiwa na faida walizozipata, hivyo, wamejiandaa kuongeza mkataba mwingine na timu hiyo.
“Ni moja kati ya udhamini ambao umetupa mapato kwa kutengeneza faida ya zaidi ya asilimia 300, naamini tukiendelea tutaweza kupata tija na faida zaidi. Tulidhamini katika muonekano sio fedha nyingi kuzidi za GSM, lakini zimewasaidia sana,†alisema Meshack na kuongeza;
“Nipongeze na nishukuru kwa ushirikiano binafsi wa Mkuu wa Mkoa kwa sababu amekuwa akiweka msukumo, nasi tunaamini timu haitashuka daraja na tutaendelea kushirikiana.â€
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo, Justine Mwandu alisema; “Wametuhakikishia na tumeona wenyewe kwahiyo tutaendelea kuidhamini labda watu wa masoko wanaweza kuona namna gani tunaweza tukaongeza huo udhamini ili kuhakikisha kwamba mkoa nao unakuwa na timu ambayo inshiriki Ligi Kuu.â€