Pamba Jiji hesabu kali mechi tatu Championship

Muktasari:

  • Katika mechi hizo tatu zilizobaki, Pamba itacheza ugenini dhidi ya Fountain Gate FC kisha itarudi nyumbani Mwanza kukipiga na TMA ambapo itamaliza mzunguko wa kwanza kwa kucheza na Mbuni FC zote hizi mbili zikipigwa Uwanja wa Nyamagana

STAA wa Pamba Jiji, Michael Samamba amesema kwa namna Ligi ya Championship ilivyo na upinzani kwa sasa kinachotakiwa kwao ni kuhakikisha wanapata ushindi katika mechi nne zilizobaki za mzunguko wa kwanza kisha baada ya hapo watajipanga kwa ajili ya raundi ya pili.

Pamba yenye maskani yake jijini Mwanza mpaka sasa imeshacheza michezo 12 ikiwa nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo imekusanya  pointi 24 ikitofautiana alama mbili na vinara wa mashindano hayo Ken Gold ambao ina 26.

Mzunguko wa kwanza wa mashindano hayo umebakisha raundi tatu kumalizika huku ligi hiyo ikionekana kuwa na ushindani mkubwa haswa kwa timu zilizo kwenye nafasi tano za juu kila mmoja akipambana ili aweze kupanda zaidi kwenye msimamo.

Katika mechi hizo tatu zilizobaki, Pamba itacheza ugenini dhidi ya Fountain Gate FC kisha itarudi nyumbani Mwanza kukipiga na TMA ambapo itamaliza mzunguko wa kwanza kwa kucheza na Mbuni FC zote hizi mbili zikipigwa uwanja wa Nyamagana.

Samamba amesema kwa sasa akili zao zipo kwenye michezo hiyo mitatu iliyobaki ambayo wanatakiwa yote kupata ushindi ambao anaamini utawaweka katika mazingira mazuri kwenye raundi ya pili ambayo huwa ngumu zaidi.

“Tumebakiza mechi tatu ili tumalize mzunguko wa kwanza hivyo ili tuwe salama inatupaswa tupate ushindi kwenye hii michezo, tunatakiwa tupambane sana maana ligi ishaanza kuwa ngumu hivyo kupata pointi tatu ni lazima ukomae mno,” amesema Samamba na kuongeza;

“Tukimaliza mzunguko huu na pointi 33 basi zitatuweka katika mazingira mazuri kwenye raundi ya pili ambayo huwa ngumu zaidi hivyo ni jukumu letu sisi wachezaji kuhakikisha tunaipambania timu kwa kufanya vizuri kwenye mechi tutakazocheza.”