Pablo baada ya ushindi wa Ruvu afunguka haya...

Kocha mkuu wa Simba Pablo Franco. Picha | Simba

BAADA ya kupata ushindi wake wa kwanza akiwa na Simba, Kocha Mkuu wa timu hiyo Pablo Franco amesema ushindi wa mabao 3-1 walioupata leo utarejesha hali ya kujiamini kwa nyota wake.

Mchezo huo ambao ni wa kwanza kwa kocha huyo amesema ameridhishwa na matokeo hayo ambayo yatawapa vijana ujasiri wa kupambana katika michezo miwili ijayo dhidi ya Geita Gold, Yanga na michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Simba imeinyuka Ruvu Shooting kwa mabao 3-1 katika Uwanja wa CCM Kirumba yakifungwa na Meddie Kagere (2), Kibu Denis na Elias Maguli akiifungia Ruvu bao la kufutia machozi.

Licha ya ushindi huo Pablo amesema hakufurahishwa na namna vijana wake walivyocheza kipindi cha pili wakishindwa kupachika bao lolote na kuruhusu bao moja.

"Bila kujali idadi ya mabao huu ushindi ni muhimu kwetu kwa sababu utarejesha hali ya kujiamini kwa vijana bado tuna mechi ziko mbele yetu na zote tunahitaji kushinda," amesema Pablo.

"Tuna michezo kama mitatu iko mbele yetu tunahitaji kufanyia kazi mapungufu lakini kiujumla nafurahishwa na wachezaji wangu wanavyowajibika uwanjani na kufanyia kazi yale tunayoyapanga japo bado safari ni ndefu lakini timu hii ina wachezaji wazuri," amesema.

Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha alama 14 nyuma ya vinara Yanga wenye pointi 14 na mchezo mmoja mkononi utakaochezwa kesho dhidi ya Namungo.