Onyango, Shikhalo wako ndaani Bongo

KENYA. Nchini Tanzania, baada ya kushuhudia mbwembwe za usajili na sherehe za ‘Simba Day’ (Simba SC) na ile ya Yanga SC ‘siku ya Mwananchi’, hatimaye wikendi kivumbi cha ligi kuu ya Tanzania (TPL), kilitimka ambapo klabu kadhaa zilijitosa uwanjani kuzindua kampeni yao!

Baada ya kushuhudia nusu ya msimu uliopita, akiwa benchi chini ya Kocha wa zamani Luc Eymael, Hatimaye siku ya Jumamosi, Kipa wa Harambee Stars, Farouk Shikhalo, alikamilisha dakika 90 langoni katika sare ya 1-1 ambayo Yanga SC iliipata dhidi ya Tanzania Prisons.

Huko Msimbazi, baada ya kukamilisha usajili kutoka Gor Mahia, Beki kisiki wa Harambee Stars, Joash Onyango alikuwa sehemu ya kwanza ya klabu ya Simba, iliyoanza kampeni ya kutetea taji lake kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Ihefu FC. Francis Kahata, hakucheza.

Mkenya mwengine, Francis Baraza, alikuwa katika kikosi cha Biashara United, kilichoanza kampeni yake vizuri, ikiondoka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Gwambina FC. Mechi hiyo, ilipigwa siku ya Jumapili. Msimu uliopita, Biashara ilimaliza ya tisa, jedwalini na pointi zake 50.