Onyango awajibu wanaomwita 'babu'

Wednesday July 21 2021
onyango pic
By Olipa Assa

BEKI wa Simba, Mkenya Joash Onyango alitaniwa sana na kupachikwa jina la 'Babu', wakati anaanza kucheza Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza, staa huyo aliamua kukausha na kuwajibu baada ya kumaliza msimu huu.

Ukitaja mabeki wa kati waliofanya kazi nzuri, huwezi kuliweka kando jina la staa huyo, jambo ambalo limempa nguvu ya kuwajibu waliokuwa wanamtania Babu, kutokana na muonekano wake ambao hata hivyo haujazuia uwezo wake.

Kabla ya Simba kucheza mechi ya mwisho dhidi ya Namungo FC, Onyango alipaka ndevu zake rangi ya udongo, alipoulizwa kwa nini ameamua kuweka urembo huo, majibu yake yalikuwa haya.

"Nimepaka rangi kwasababu mimi ni babu dhidi ya wengine ni hivyo tu sina lingine zaidi ya hilo," alijibu kwa kifupi Onyango ambaye amekuwa panga pangua katika kikosi cha kwanza cha kocha wake Didier Gomes.

Ingawa sio mara ya kwanza kwa Onyango kupaka rangi katika ndevu zake, aliwahi kuonekana na muonekano wa rangi nyeupe akiwa na timu yake ya zamani ya Gor Mahia ya Kenya.

Kabla ya kupaka awamu hii, Onyango aliwahi kuelezea kwamba hawezi kupingana na kila shabiki anayempachika jina na kwamba ndio kazi yao.

Advertisement

"Kazi yangu mimi ni kucheza na kuonyesha nilichonacho, kazi ya shabiki ni kushangilia ama kuzomea, hivyo sishangazwi na majina yao, nipo huru waniite watakavyo,"amesema.

Advertisement