Onyango akabidhiwa mkwanja, tuzo Simba

Monday April 05 2021
onyango pic tuzo 2
By Ramadhan Elias

BEKI kisiki wa Simba, Joash Onyango amekabidhiwa tuzo yake ya mchezaji bora wa mwezi Machi klabuni hapo na Ofisa masoko na mawasiliano wa kampuni ya Emirate Aluminium Profile, Issa Maeda.

Onyango alishinda tuzo hiyo kwa mwezi uliopita kwa kuwapiku golikipa Aishi Manula na Luis Miquissone ambao waliingia naye kwenye kinyang’anyiro cha tatu bora.

onyango pic tuzo

Tuzo hizo zinapigiwa kura na mashabiki katika mitandao ya kijamii ya Facebook, Twitter na Instagram ambapo mchezaji mwenye kura nyingi kati ya waliopendekezwa ndiye anakuwa mshindi.

Kwa mujibu wa waandaaji wa tuzo hizo, Simba pamoja na Emirate Aluminium Profile, Onyango amewashinda wenzake kwa uwiano wa asilimia 79% akifuatiwa na Manula aliyepata 18% na Miquissone asilimia tatu.

Baada ya kupokea tuzo hiyo Onyango amewashukuru mashabiki kwa kumpigia kura na kuwaahidi kuendelea kupambana kwajili ya Simba.

Advertisement

“Natoa shukrani zangu kwa mashabiki wote walionipigia kura kuwa mchezaji bora wa mwezi huu pia nawaahidi kuendelea kupambana kwajili ya Simba na na nitashirikiana na wachezaji wenzangu ili kutimiza malengo ya klabu,” amesema Onyango.

Tuzo hizo zilianzishwa mwezi Februari na mshindi alikua Luis Miquissone hivyo Onyango ni mshindi wa awamu ya pili akibeba mwezi huu.

Advertisement