Onyango aitabiria makubwa Simba CAF, Bocco mdogo mdogo

Muktasari:

  • Onyango alisema kutokana na kuweka kwao mikakati kutawasaidia kufanya vizuri zaidi katika mashindano hayo.

BEKI kisiki wa Simba, Joash Onyango amesema anaiona timu yake katika fainali za Ligi ya Mabingwa msimu huu.

Onyango aliyasema hayo wakati anakabidhiwa tuzo ya mchezaji bora wa Machi zinazotolewa na kampuni ya Emirates Aluminium Profile kwa kupigiwa kura na mashabiki wa klabu hiyo katika mitandao ya kijamii.

Beki huyo alisema wao kama wachezaji walianza na ndoto ya kufuzu katika hatua ya makundi kwa kuhakikisha kila mchezo wanapata ushindi katika hatua hiyo.

“Kwenye hatua ya makundi tulikuwa na malengo ambayo kocha alituwekea kushinda kila mchezo uliopo mbele yetu, kwahiyo hata huo ujao licha ya kufunga bado ni mchezo wenye uzito kwetu”.

“Tumefuzu na tunajua kabisa tunaenda kukutana na timu ngumu lakini tunaenda kupambana na naamini kabisa tutaenda nusu fainali mpaka fainali”.

Akizungumzia kwa upande wake umuhimu wa Ligi ya Mabingwa, alisema imemuongezea vitu vingi katika uchezaji wake.

“Huku nakutana na wachezaji kutoka mataifa tofauti kwahiyo lazima ubora kwangu uongezeke” alisema kwa kifupi.

MAZOEZI SAFI, BOCCO MDOGO MDOGO

Simba jana Jumatatu iliendelea na mazoezi baada ya kutoka katika mapumziko mafupi ya sikukuu ya pasaka, walifanya mazoezi asubuhi katika uwanja wao wa Bunju.

Katika mazoezi hayo kocha Didier Gomes ni kama alikuwa anawapa mazoezi mepesi ya kunyoosha misuli kwa wachezaji hao.

Aliwataka wachezee mpira kwa muda mrefu huku akiwapanga kwa mafungu wachezaji hao na baadaye aliwapumzisha na kubaki na kundi moja.

Gomes aliwapanga Beno Kakolanya, Kennedy Juma, Gadiel Michael, Mzamiru Yassin, Hassan Dilunga na Erasto Nyoni.

Upande mwingine ukiwa na Ally Salim, David Kameta ‘Duchu’ Benard Morrison, Said Ndemla, Ibrahim Ame na Ibrahim Ajibu.

Katika mazoezi hayo alikuwa anawataka wachezaji wake wawe wepesi katika kupiga pasi huku wakielekea langoni.


BOCCO APEWA ZOEZI MAALUM

Mshambuliaji John Bocco yeye alipewa programu maalum na kocha wa viungo, Adel Zerane muda wote ambao wenzake walikuwa wanacheza.

Mshambuliaji huyo alikuwa anakimbizwa kwa kuhesabiwa dakika lakini alitakiwa kutumia spidi muda wote.

Bocco hakuonyesha kutegea zoezi hilo ambalo alikuwa anasimamiwa na Zerane alipokuwa anafanya kwa umakini.