Saido amaliza utata Yanga

Muktasari:

MASHABIKI wa Yanga waliokuwa na presha kubwa juu ya staa wao, Saido Ntibazonkiza ambaye hajaonekana uwanjani kwa muda mrefu na timu hiyo tangu awe majeruhi, wanywe na kunywa kwa raha zao kwani jamaa amerudi kwa kishindo na kumaliza utata uliokuwapo.

MASHABIKI wa Yanga waliokuwa na presha kubwa juu ya staa wao, Saido Ntibazonkiza ambaye hajaonekana uwanjani kwa muda mrefu na timu hiyo tangu awe majeruhi, wanywe na kunywa kwa raha zao kwani jamaa amerudi kwa kishindo na kumaliza utata uliokuwapo.

Saido alizua sintofahamu ya kwamba huenda asingerejea baada ya kuwa majeruhi wa muda mrefu na kuchomolewa kwa Kocha Cedric Kaze aliyependekeza asajiliwe, lakini mshambuliaji huyo aliyekuwa na timu ya taifa ya Burundi, amerudi ila akakaribishwa na shoo ya kibabe ya wachezaji wenzake mpaka akakimbia uwanjani.

Ipo hivi. Saido alitua nchini usiku wa Ijumaa kimyakimya akitokea kwao na haraka juzi Jumamosi akaibukia kambini mchana kujiunga na wenzake bila kumpa taarifa bosi yeyote kwani wakishtukia jamaa akivuta kiti na kuangalia mazoezi ya wenzake.

Mwanaspoti lililomshuhudia mshambuliaji huyo mazoezini hapo, lakini hakutaka kuongea kitu zaidi ya kuwaangalia wenzake wakijifua kwa mechi ya wao kwa wao katika kujiweka sawa.

Hatua ya kurejea kwa Saido kunarudisha mzuka zaidi kwa mashabiki wa Yanga waliokuwa na wasiwasi na staa wao huyo aliyeonekana na uzi wa timu yao uwanjani kwenye mechi ya Fainali ya Kombe la Mapinduzi 2021 alipopiga penalti ya ushindi na kubeba ubingwa dhidi ya Simba kwenye mechi iliyopigwa Januari 13, visiwani Zanzibar.

Baada ya kuwa nje kwa muda mrefu, Saido liitwa timu ya Burundi kwa mechi za kirafiki na zile za kuwania kufuzu fainali za Afrika 2021, huku kocha Kaze wakati huo akiinoa Yanga akilalamika kwa kutoshirikishwa kuitwa kwake, kwa vile hakuwa amepona vyema, japo akiwa na timu hiyo alifunga. bao.

Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga,Juma Mwambusi akizungumzia kurejea kwa Saido, alisema kutaongeza mzuka zaidi katika timu yakena sasa wanamsubiri mtu mmoja kukamilisha jeshi lao.

“Saido amewasili, hii ni hatua muhimu kwetu, tunaamini sasa amepona na anakuja kuendeleza kazi yake akishirikiana na wenzake ambao nao wameshawasili. Kwa sasa mchezaji aliyesalia ni Haruna Niyonzima, naye akitua tu kila kitu kitakuwa freshi,” alisema Mwambusi na kuongeza;.

“Timu ikikamilika hivi lazima kama kocha upate furaha na jambo zuri karibu wote wamewasili wakiwa salama na leo tulikuwa tunawaangalia wamerejea kwa ubora gani. Tuna siku kadhaa za kufanya mazoezi kwa pamoja ili tuwe tayari kwa mchezo wetu wa kwanza dhidi ya KMC, tutakuwa na maandalizi kabambe kuelekea mchezo huo.”

Yanga itarejea katika Ligi Kuu Bara kwa kuvaana na KMC, Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mechi ya kisasi kwa timu hizo, kwani walipokutana mara ya mwisho kwenye Uwanja huo Machi 12, mwaka jana, Yanga ilicharazwa bao 1-0.

Kipigo hicho ndicho kilichokuwa pekee kwa Yanga na kucheza michezo i 33 bila kupoteza kabla ya Coastal Union kuitibulia hivi karibuni kwa kuwafunga mabao 2-1 jijini Tanga.

Pia kwenye mchezo wao wa kwanza uliopigwa jijini Mwanza, KMC walilala mabao 2-1.