Gomes kuwasapraizi Waarabu

Muktasari:

LICHA ya kujihakikishia kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na pia uongozi wa kundi A, Kocha wa Simba, Didier Gomes Da Rosa amepanga kuisapraizi zaidi Al Ahly watakaovaana nao Ijumaa hii kwa kutumia kikosi chake kamili kama ilivyokuwa kwenye mchezo wao wa kwanza jijini Dar es Salaam na kuwafumua bao 1-0.

LICHA ya kujihakikishia kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na pia uongozi wa kundi A, Kocha wa Simba, Didier Gomes Da Rosa amepanga kuisapraizi zaidi Al Ahly watakaovaana nao Ijumaa hii kwa kutumia kikosi chake kamili kama ilivyokuwa kwenye mchezo wao wa kwanza jijini Dar es Salaam na kuwafumua bao 1-0.

Kwa vile Simba haina cha kupoteza katika mchezo huo, ilitegemewa benchi lake la ufundi kutoa nafasi kwa kundi kubwa la wachezaji ambao hawajatumika sana katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu hasa hatua ya makundi, lakini Kocha Gomes na benchi lake la ufundi wameamua kuivaa Al Ahly na kikosi chao kilichozoeleka lengo wakitaka kumaliza kwa kishindo hatua ya makundi ambayo wameonekana kuwa tishio.

“Ni jambo la kufurahisha kuona tumepata ushindi muhimu dhidi ya AS Vita Club na sasa ni rasmi tutaongoza msimamo wa kundi na tumefuzu hatua ya robo fainali ya mashindano haya. Niwapongeze wachezaji wangu kwa kazi nzuri waliyofanya licha ya wengi wao kufanya mazoezi na timu kwa muda mfupui kutokana na majukumu waliyokuwa nayo katika timu za taifa.

Tuna mchezo ulio mbele yetu dhidi ya Al Ahly. Ni mchezo ambao tunahitaji kupata matokeo mazuri na malengo yetu ni kutumia kikosi chetu kamili katika mchezo huo na sio kufanya mabadiliko makubwa kwani tunahitaji kushinda.

Hata hivyo hilo litategemea na hali za wachezaji kuelekea katika mchezo huo kwani kuna muda wa takribani wiki upo mbele yetu hivyo tutaangalia itakavyokuwa,” alisema Gomes.

Akizungumzia ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya AS Vita Club ambao umeifanya Simba iweke rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kumaliza hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika ikiwa kinara, Gomes alisema ni jambo zuri lililotokana na juhudi kubwa za wachezaji wake.

“Kwa mara nyingine nasema, wachezaji wangu wameonyesha weledi wa hali ya juu, wanajituma na pia wana uvumilivu. Binafsi nina furaha kubwa kuona tumefuzu hatua ya robo fainali huku tukiwa tunaongoza kundi. Nawapongeza wachezaji, viongozi, mashabiki na wenzangu katika benchi la ufundi kwa hiki tulichokipata.

Kwa sasa tunaingia katika hatua ngumu ambayo tunahitajika kufanya maandalizi mazuri ili tuweze kusonga mbele na kufika hatua za juu zaidi,” alisema Gomes.

Chini ya Gomes, Simba imeonekana kuwa tishio katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ambapo ndio timu pekee ambayo haijapoteza mechi yoyote ya hatua ya makundi, ikipata ushindi katika mechi nne na kutoka sare moja kati ya tano ilizocheza.

Simba ndio timu ambayo imekuwa na ukuta wa chuma kwani katika raundi tano za hatua ya makundi, imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja tu na kiujumla katika mashindano hayo msimu huu, imefungwa mabao mawili tu.