Ole hajafunga duka Man United

MANCHESTER,ENGLAND.HABARI ndio hiyo. Manchester United inasubiri tu dirisha la usajili la Januari na lile la mwisho wa msimu kufanya mambo yao kuhakikisha wanafanya marekebisho makubwa kwenye kikosi chao.

Baada ya kushindwa kufanya usajili mkubwa sana kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka huu, kocha Ole Gunnar Solskjaer bado mipango yake ya usajili ipo kwa wachezaji walewale ambao atahitaji kuwa na huduma zao huko Old Trafford.

Pengine Januari inaweza kupita bila ya kufanya usajili wowote mkubwa, lakini Man United imepanga kufanya biashara ya kibabe usajili wa majira ya kiangazi mwakani kwa kuhakikisha inanasa saini za mastaa straika Erling Haaland, winga Jadon Sancho na beki wa kati Dayot Upamecano.

Solskjaer alijaribu kufanya usajili wa Haaland Januari mwaka huu, lakini ikashindikana na staa huyo alitimkia zake Borussia Dortmund. Hata hivyo, kwenye mkataba wake kuna kipengele kinachohitaji kulipiwa Pauni 68 milioni pekee kuvunjwa kitu ambacho Solskjaer amepanga kukifanya dirisha litakapofunguliwa, huku mchezaji mwenyewe akimzungumzia kocha huyo na kuweka wazi milango ya kutoa Old Trafford.

Haaland alisema: ìSolskjaer amekuwa na mchango mkubwa sana katika maisha yangu, kama mwanadamu na kama kocha. “Alishinda Ligi ya Mabingwa Ulaya na alikuwa mchezaji mahiri. Amenifundisha mambo mengi sana.”

Kisha aliongeza: “Nimekuwa na ndoto za kuchezea klabu kubwa katika maisha yangu, hasa klabu za England.” Kuhusu Upamecano, kocha Solskjaer amekiri kumfuatilia mchezaji huyo huku akiamini atatumia mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya wa jana Jumatano usiku dhidi ya Red Bull Leipzig kumtazama kwa ukaribu zaidi beki huyo.

“Tunajaribu kuheshimu kwamba huyu ni mchezaji wa timu nyingine, hivyo nisingependa kuongea sana kuhusiana na mchezaji ambaye tumekuwa tukihusishwa naye,” alisema.

“Lakini, kwa sababu tunacheza mechi dhidi yake, nadhani ni nafasi nzuri ya kumtazama kwa ukaribu zaidi.” Kuhusu ishu ya Sancho, ambaye alihusishwa sana kutua Old Trafford kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi, kocha wake wa Dortmund, Lucien Favre amedai kwamba tangu dili la winga huyo Mwingereza kwenda Man United kushindikana kiwango chake kimeshuka ndani ya uwanja.