Okoyo siyo soka tu hata gitaa freshi

Muktasari:
- Okoyo alisema endapo ndoto ya soka isingetimia, basi angekuwa mwanamuziki kwani ni kitu alichokuwa anakipenda tangu utotoni.
KIUNGO wa kati wa KMC, Deusdedity Cosmas Okoyo amesema nje na kucheza soka ni mtaalamu wa kupiga gitaa linalomsaidia kumpa utulivu anapopata muda wa kupumzika baada ya mechi.
Okoyo alisema endapo ndoto ya soka isingetimia, basi angekuwa mwanamuziki kwani ni kitu alichokuwa anakipenda tangu utotoni.
“Zamani nilikuwa napenda kuimba sana, nikajifunza kupiga gitaa ambalo hadi sasa wakati mwingine nikitoka kwenye mechi ama mazoezini nikitulia chumbani nalipiga na linanisaidia kupata utulivu wa akili,” alisema Okoyo na kuongeza:
“Nilipoona milango ya soka imefunguka nikaachana na mambo ya kuimba nikaweka nguvu katika mazoezi ili niwe naonyesha kiwango kizuri uwanjani, hivyo sitarajii kuipigania ndoto ya kuwa msanii tena.”
Alitolea mfano wa msanii wa Bongo Fleva, Alikiba kwamba alianza na ndoto ya soka, lakini ilipotimia ya kuimba na sasa amekuwa kioo cha vijana wengi kutamani kuyafikia mafanikio yake.
“Ukiwauliza watu wengi maarufu kabla ya hicho kilichowatoa walikuwa na ndoto nyingine ambazo zilishindwa kutimia,” alisema Okoyo ambaye hana asisti wala bao katika Ligi Kuu Bara msimu huu ambao amejiunga na KMC baada ya kukaa nje ya uwanja mwaka mzima alipoumia akiwa na JKT Tanzania.