Nyota waliowahi kukipiga Barcelona na Man United

Muktasari:

  • Wafuatao ni mastaa ambao wamewahi kukipiga katika klabu zote mbili hizi.

BARCELONA,HISPANIA.BARCELONA na Manchester United leo wanaamua hatima ya nani kati yao aende katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.

Wafuatao ni mastaa ambao wamewahi kukipiga katika klabu zote mbili hizi.

Mark Hughes

Ni moja kati ya zao la soka la watoto Manchester United mwanzoni mwa miaka ya 1980. Baadaye akaichezea United mechi ya kwanza mwaka 1983. Mshambuliaji huyu ambaye kwa sasa ni kocha alifanya mambo makubwa katika misimu yake mitatu ya kwanza aliyokipiga Old Trafford. Hughes hatimaye alinunuliwa na Barcelona mwaka 1986 kwa dau la Pauni 2 milioni. Hata hivyo, msimu wake wa kwanza ulikwenda hovyo na mwishoni mwa msimu alipelekwa kwa mkopo Bayern Munich.

Mei 1988 alinunuliwa tena na Sir Alex Ferguson kwa rekodi ya klabu Pauni 1.8 milioni. Akawa mchezaji muhimu katika kikosi cha United huku akitwaa mataji mawili ya Ligi Kuu ya England, matatu ya FA, moja la washindi na jingine la Super Cup.

Jordi Cruyff

Mtoto wa staa wa zamani wa Barcelona na timu ya taifa ya Uholanzi, Johan Cruyff. Jordi alikulia Barcelona B na kuichezea Barcelona ya wakubwa mechi ya kwanza Septemba 1994. Alicheza misimu miwili akiwa na wababe hao wa Catalunya kabla ya kuamua kutua Manchester United.

Kipindi chake England kilitawaliwa na majeraha ya mara kwa mara na akapelekwa kwa mkopo Celta Vigo katikati ya msimu ambao United walitwaa mataji matatu mwaka 1999. Hata hivyo, kabla ya hapo mwaka 1997 alifanikiwa kuvaa medali ya ubingwa wa England.

Laurent Blanc

Mmoja kati ya walinzi bora wa muda wote Ulaya na alitwaa Kombe la Dunia mwaka 1998 na kikosi cha Ufaransa kabla ya kutwaa Euro 2000. Katika ubora wake alicheza timu kubwa tisa tofauti barani Ulaya huku mbili kati ya hizo zikiwa ni Barcelona na Manchester United.

Alitua Barcelona mwaka 1996 kutokana na tamaa yake ya kucheza chini ya kocha mkongwe, Johan Cruyff. Hata hivyo, Cruyff alifukuzwa mara tu baada ya Blanc kuwasili. Blanc aliishia kucheza mwaka mmoja tu. Alijiunga na Manchester United mwaka 2001 huku ubora wake ukianza kupungua. Hata hivyo, aliondoka na medali moja ya ubingwa wa England katika msimu wake wa pili akiwa na United. Msimu uliofuata alistaafu soka.

Henrik Larsson

Mmoja kati ya wachezaji bora wa muda wote katika soka la Sweden. Baada ya kuhakikisha mkataba wake na Celtic unamalizika hatimaye Larsson alihamia Barcelona bure mwaka 2004. Msimu wake wa kwanza alikumbwa zaidi na majeraha lakini msimu wa pili alitesa zaidi. Alipika mabao mawili ambayo yaliisaidia Barcelona kuichapa Arsenal 2-1 na kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2006.

Baada ya mkataba wake kumalizika aliondoka Barcelona bure na kurudi kwao Sweden kukipiga katika klabu ya Helsingborg. Wakati ligi ya Sweden ilipokwenda mapumziko alikwenda Manchester United kucheza kwa mkataba wa miezi miwili kuanzia Januari hadi Machi 2007. Aliichezea Manchester mechi 13 tu katika michuano mbalimbali lakini Sir Alex Ferguson alihakikisha kwamba anapokea medali ya ubingwa.

Gerard Pique

Pamoja na kwamba alikuwa amekulia Barcelona katika soka la vijana lakini Gerard Pique alisaini mkataba wake wa kwanza wa soka la kulipwa akiwa na Manchester United na hatimaye kucheza mechi ya kwanza katika kikosi hicho Oktoba 2004.

Mlinzi huyu wa kati alitwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England, Ngao ya Hisani na kisha ubingwa wa Ulaya akiwa na Manchester United kabla ya kurudi Barcelona mwaka 2008. Kwa sasa yupo katika msimu wake wa 11 Nou Camp na tayari Pique ametwaa mataji ya kutosha pale Barcelona huku akiwa mmoja kati ya mastaa wanaoheshimika zaidi.

Victor Valdes

Mwanafunzi mwingine katika shule ya soka ya Barcelona. Valdes aliichezea Barcelona mechi ya kwanza Agosti 2002, lakini alilazimika kusubiri mpaka msimu wa 2003-04 kuwa chaguo la kwanza.

Ni nchini Hispania ndipo alipotesa zaidi huku akitwaa mataji sita ya La Liga na matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Aliondoka Barcelona mwishoni mwa msimu wa 2013-14 na Oktoba 2014 Manchester walimpa nafasi ya kufanya matibabu katika klabu yao na kisha Januari 2015 alisaini mkataba wa miezi 18. Hata hivyo, alicheza mechi mbili tu kabla ya kuondolewa na kocha Louis van Gaal Januari 2016.

Zlatan Ibrahimovic

Mmoja kati ya mastaa ambao wamesafiri sana kucheza katika klabu mbalimbali tofauti. Alijiunga na Barcelona mwaka 2009 katika uhamisho wa kubadilishana na Samuel Eto’o akitokea Inter Milan. Licha ya kutua akiwa na jina kubwa pale Barcelona lakini uhusiano wake na kocha, Pep Guardiola haukuwa mzuri huku pia Pep akimchezesha pembeni kwa ajili ya kumpanga Lionel Messi katikati. Ugomvi wake na Guardiola ulisababisha aondoke klabuni hapo ndani ya msimu mmoja tu. Baadaye akatolewa kwa mkopo kwenda AC Milan na baadaye akauzwa jumla katika klabu hiyo ya Italia. Alijiunga na Barcelona kwa uhamisho wa bure Julai 2016 akitokea PSG ambako alimaliza mkataba. Zlatan alifanya mambo makubwa katika msimu wake wa kwanza chini ya kocha, Jose Mourinho ambaye ni kocha wake wa zamani Inter Milan. Alitwaa mataji matatu likiwamo taji la Europa. Hata hivyo, mwishoni mwa msimu wake wa pili aliumia vibaya goti lake na United waliamua kukatisha mkataba wake Machi 2018.

Alexis Sanchez

Ni miongoni mwa mastaa wa Manchester United ambao wamesafiri kucheza pambano la leo pale Nou Camp. Anarudi katika uwanja wake wa zamani baada ya awali kuichezea timu hii akihamia kutoka Udinese Julai 2011. Kwa kuhamia kwake Nou Camp wakati huo aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Chile kucheza Barcelona.

Alicheza kwa mafanikio katika misimu yake mitatu kando ya mastaa Lionel Messi na David Villa. Hata hivyo, kuwasili kwa Neymar mwaka 2014 kulisababisha Sanchez aondoke zake na kutimkia Arsenal.

Baada ya misimu mitatu na nusu akiwa na Arsenal, Sanchez aliamua kuruka boti na kutua Manchester United kwa uhamisho wa kubadilishana na staa Henrikh Mkhitaryan.

Alipewa jezi namba 7 ambayo kwa bahati mbaya mpaka leo hajaitendea haki. Kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa Sanchez hajaweza kurudia makali yake aliyoonyesha akiwa na klabu za Udinese, Barcelona na Arsenal.