Nyota Mtibwa Sugar watua Geita Gold
Muktasari:
- Baada ya Mtibwa Sugar kushuka daraja mastaa wake wengi wameonekana kujiunga na timu kadhaa kwenye ligi jambo ambalo linaonyesha hofu kubwa kwa timu hiyo kwenye ligi ya Championship msimu ujao.
TIMU ya Geita Gold iliyopanda kucheza Ligi Kuu Bara msimu unaotarajia kuanza Agosti 14, 2026, inadaiwa kuwasajili nyota wa Mtibwa Sugar, kiungo Twalibu Muhenga na beki wa kulia Datius Peter.
Chanzo cha ndani kutoka Geita Gold kilisema kuna wachezaji ambao wataachwa na wengine kusajiliwa, ili kupata kikosi imara chenye ushindani kwa ajili ya ligi ijayo.
Baada ya Mtibwa Sugar kushuka daraja mastaa wake wengi wameonekana kujiunga na timu kadhaa kwenye ligi jambo ambalo linaonyesha hofu kubwa kwa timu hiyo kwenye ligi ya Championship msimu ujao.
“Miongoni mwa wachezaji ambao viongozi wameshawasajili ni nyota wa Mtibwa iliyoshuka daraja, Muhenga na Peter na bado inaendelea kufanya mazungumzo na wengine,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Ukiachana na hao, kuna wachezaji ambao walishamaliza mikataba yao na viongozi wanafanya mazungumzo ya kuwapa mikataba mipya, jambo la msingi zaidi timu ikikamilisha usajili itatoa taarifa rasmi.”
Alipotafutwa Mhilu kuzungumzia hilo amesema: “Kwa sasa siwezi kuzungumza chochote, lakini kila kitu kikiwa sawa basi wahusika ndio wanaojua utaratibu wa kuwatangaza wachezaji wao.”
Kwa upande wa Peter amesema: “Timu nitakayoichezea msimu ujao itajulikana utakapofika wakati sahihi, ila kwa kipindi hiki sina jibu lolote la kukupa.”