Nyie...Jidanganyeni!

Muktasari:

YANGA imezisikia kelele zinazoendelea mtaani kwa mashabiki wa Simba kujiaminisha kwamba chama lao litawalaza mapema Wanajangwani katika mechi yao ya Kariakoo Derby, kisha wakacheka sana na kuwaambia watani wao hao; ‘Nyieee, jidanganyeni tu muone’.

YANGA imezisikia kelele zinazoendelea mtaani kwa mashabiki wa Simba kujiaminisha kwamba chama lao litawalaza mapema Wanajangwani katika mechi yao ya Kariakoo Derby, kisha wakacheka sana na kuwaambia watani wao hao; ‘Nyieee, jidanganyeni tu muone’.

Sio kusema hivyo tu, lakini vigogo wake wakaamua kuzuga wakitaka kucheza na akili za Simba kwa kusema kuwa, mchezo huo wa Jumamosi ambao ni wa 106 kwao kukutana katika Ligi ya Bara tangu 1965 ni mgumu kuliko hata zilizopita, kwani Simba itataka kulipa kisasi cha aibu.

Simba watakuwa wenyeji wa Yanga kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam ikiwa ni miezi kama minne tangu walipokutana katika fainali ya Kombe la Mapinduzi 2021 visiwani Zanzibar na Jangwani kuwatambia watani wao kwa kuwafunga kwa mikwaju ya penalti.

Pambano hilo linakuja baada ya sare ya 1-1 kwenye duru la kwanza, huku mechi mbili za msimu uliopita za Ligi Kuu, Simba ikiambulia pointi moja tu kati ya sita kutokana na sare ya 2-2 ya mchezo wa kwanza uliopigwa Januari 4 mwaka jana kisha kupasuka bao 1-0 katika mechi iliyopigwa Machi 8, pia mwaka jana.

Simba tayari wamelianzisha huko mtaani na kwenye mitandao ya kijamii, huku baadhi ya viongozi wake wakitamba kuwa, kwa mziki walionao kwa sasa hawaoni kwanini wasichukue pointi tatu ili kujiweka pazuri kwenye mbio za kutetea ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo.

Lakini, Mtendaji Mkuu wa zamani wa Simba aliye Mshauri Mkuu wa Yanga kwa sasa, Senzo Mazingisa ameliambia Mwanaspoti kuwa ni kweli mechi hiyo ya Jumamosi ni ngumu na itakayotoa taswira ya mbio za ubingwa huku akisisitiza Simba wasijidanganye.

Senzo alikiri ni kweli mechi hiyo ni ngumu kwelikweli na ugumu upo kwa timu zote kutokana na mazingira yanayowakutanisha kwa sasa, akiamini wapinzani wao watakuwa wakitaka kulipa kisasi cha kufungwa kwenye Kombe la Mapinduzi na kushindwa kupata ushindi katika mechi zao tatu zilizopita za Ligi Kuu walipokutana

“Tuliwafunga kwenye Kombe la Mapinduzi, tukaja tukatoka nao sare kwenye mchezo wa raundi ya kwanza, lakini mechi mbili za msimu uliopita walishindwa kupata matokeo ni wazi naona kabisa safari hii watahitaji kulipa kisasi na ndipo ugumu utakapokuwepo,” alisema Senzo kama mtu anayecheza na akili za Simba akisema ushiriki wao wa mechi za kimataifa ni faida nyingine kwao.

“Ugumu mwingine wa mchezo huu ni kwamba ukiangalia tupo kwenye mbio za ubingwa na tunafukuzana kwenye msimamo, wenzetu wakiongoza na sisi tukifuata kwa tofauti ndogo tu,” alisema.

Senzo alisema kwa namna pambano la watani linavyokuwa, licha ya vikosi vyote kuwa na wachezaji mahiri na wenye vipaji, lakini kitakachoamua matokeo ni jinsi walivyojiandaa akisisitiza hata wao wapo makini kuhakikisha wanajiandaa ili kuwakabili watani wao.

Alisema ushindi wao wa mchezo uliopita wa michuano ya ASFC, umeongeza morali kubwa kwa kikosi chao.

“Morali kwa upande wetu imeongezeka baada ya kupata ushindi katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons, awali tulikuwa hatupo vizuri sana lakini morali imerejea kwa wachezaji.”

Yanga iliifunga Prisons 1-0, huku watani wao wakishinda mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar na zote kutinga robo fainali na kufanya timu zote kukutana zikiwa na morali zaidi katika derby.

Katika mechi 105 za awali zilizokutanisha timu hizo katika Ligi ya Bara tangu 1965, Yanga imeshinda jumla ya mechi 37, huku Simba ikishinda 31 na sare 37.