Novatus kuweka rekodi mpya UEFA

Muktasari:

  • Huu utakuwa mchezo wa tano kwa timu hizi mbili kukutana kwenye Ligi ya Mabingwa, huku FC Porto ikionekana kuwa na rekodi nzuri kwani imeshinda na kutoka sare mara mbili hivyo FC Shakhtar Donetsk itakuwa ikisaka ushindi wake wa kwanza.

NYOTA wa Kitanzania, Novatus Dismas anatarajiwa leo, Jumanne kuwa sehemu ya kikosi cha FC Shakhtar Donetsk ambacho kitakuwa nyumbani kwenye uwanja wao wa National Sports Complex kwa ajili ya kutupa karata yao ya kwanza kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya FC Porto ya Ureno.

Huu utakuwa mchezo wa tano kwa timu hizi mbili kukutana kwenye Ligi ya Mabingwa, huku FC Porto ikionekana kuwa na rekodi nzuri kwani imeshinda na kutoka sare mara mbili hivyo FC Shakhtar Donetsk itakuwa ikisaka ushindi wake wa kwanza.

Shakhtar Donetsk itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na rekodi nzuri ya kutopoteza ikiwa nyumbani katika mchezo wa ushindani mwaka huu.

Akiongelea mchezo huo, kocha wa Shakhtar, Patrick van Leeuwen alionyesha kuiheshimu FC Porto kwa kusema wanajua kuwa ni timu nzuri na bora lakini wapo tayari kukabiliana nao kulingana na maandalizi waliyofanya.

“Utakuwa mchezo mzuri na wa kuvutia kulingana na ubora wa wapinzani wetu lakini sisi ni Shakhtar, tutapambana mbele ya mashabiki wetu ambao siku zote wamekuwa nyuma yetu kuhakikisha tunakuwa na mwanzo mzuri,” alisema kocha huyo.

Patrick ana maingizo kadhaa mapya kwenye kikosi chake ikiwemo mchezaji kinda wa Kitanzania, Novatus ambao taratibu amekuwa akiwapa nafasi kuanzia kwenye michezo ya kirafiki baada ya wiki ya kimataifa ili kuzoeana na wachezaji wenzao ikiwa ni hatua chache kabla ya kuanza kuwatumia.

Katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Ukraine ambao Shakhtar ilikuwa nyumbani kucheza dhidi ya Obolon, Novatus alikuwa miongoni mwa wachezaji wa akiba huku kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Blago-Youth akipata nafasi ya kucheza.

Shakhtar sio wanyonge kwenye soka la Ulaya kwani 2009, ilikuwa timu ya pili ya Ukraine kushinda taji la Ulaya (na ya kwanza tangu uhuru), na ya kwanza kushinda Kombe la UEFA baada ya kuwashinda Werder Bremen katika fainali, kwa mabao ya Wabrazili Luiz Adriano na Jadson.