No retreat, No Surrender

Mashabiki wa timu ya Yanga wakishangilia jukwaani. Picha na Maktaba
Muktasari:
Simba wakafurahia ujio wa mchezaji huyo kwa vile anacheza kwa mapenzi zaidi akiwa kwao, lakini wenzao wa Yanga bado wakawa na mawazo kutokana na maneno ya mitaani pamoja na mamilioni ya shilingi ambayo Okwi alizoa kiulaini.
YANGA ilimsajili Emmanuel Okwi msimu uliopita kwa lengo la kuboresha fowadi yake, lakini baadaye mchezaji huyo akatofautiana na timu hiyo na kufuata taratibu za kisheria akarejea kwenye timu yake ya zamani, Simba ambayo leo Jumamosi inacheza na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Simba wakafurahia ujio wa mchezaji huyo kwa vile anacheza kwa mapenzi zaidi akiwa kwao, lakini wenzao wa Yanga bado wakawa na mawazo kutokana na maneno ya mitaani pamoja na mamilioni ya shilingi ambayo Okwi alizoa kiulaini.
Okwi baada ya kukamilisha usajili wake Simba akawaambia Yanga akisema: “Yanga msije uwanjani Oktoba 18.” Kauli yake inamaanisha kwamba leo atawadhalilisha.
Straika Mbrazili Genilson Santos ‘Jaja’ aliposikia maneno yamezidi na watu wanambeza akaipiga Azam mabao mawili kwenye mechi ya Ngao ya Jamii na ilikuwa kama anawauliza mashabiki akisema: “Okwi wa kazi gani?”
Kama hiyo haitoshi, Andrey Coutinho aliposikia makelele hayo akawaambia mashabiki wa Yanga kwa ishara kwamba mambo yake yataonekana uwanjani hazungumzi sana. Hayo ndiyo kati ya mambo yatakayonogesha mechi hiyo ambayo kila upande umekoki silaha zake na kutamka kwamba ‘No Retreat, No Surrender’ wakimaanisha kwamba ‘Hakuna kujisalimisha wala kurudi nyuma’ bali lazima kieleweke ndani ya dakika 90.
Yanga yenye Wabrazili wanne akiwamo Kocha Mkuu, Marcio Maximo inakutana kwa mara ya kwanza msimu huu na Simba ya kocha mwenye uwezo mkubwa wa kusoma na kudhibiti mchezo, Mzambia Patrick Phiri.
Maximo na Phiri wamewaambia mashabiki wa soka nchini waache nongwa, waelekee uwanjani kushuhudia soka la aina yake ambalo halijawahi kuonekana tangu msimu huu uanze.
YANGA
Mbali na mazoezi mengine, Yanga imekuwa na siku tano za programu maalumu ya maandalizi dhidi ya Simba ambazo zimekamilika jana Ijumaa.
Kikosi hicho kiliweka kambi eneo la Kunduchi katika hoteli ya Landamark na kufanyia mazoezi yake katika Uwanja wa Boko Veteran.
Kwa wiki nzima, Maximo amekuwa akicheza na akili za wachezaji wake kwa kufanya vikao visivyo rasmi ikiwa ni njia ya kuwatengeneza kisaikolojia, jambo ambalo limekuwa likiongeza ufanisi na kupandisha morali kwa kikosi hicho kilichoshika nafasi ya pili msimu uliopita.
Awali viongozi pamoja na mashabiki wa Yanga walikumbwa na taharuki baada ya nahodha wa timu, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kupata majeraha kwenye mechi kati ya Taifa Stars na Benin, lakini kwa sasa ameonekana kuimarika hasa baada ya kupata ruhusa ya kucheza kutoka kwa Daktari wa timu hiyo, Juma Sufiani.
Hakuna mchezaji wa Yanga aliyepokonywa simu, ni tofauti na ilivyofanywa na viongozi wa Simba kwa wachezaji wao, lakini uongozi wa Yanga chini ya Kamati ya Mashindano inayoongozwa na Mhandisi Issac Chanji na wenzake Seif Ahmed, Musa Katabaro na Abdalah Bin Kleb, jana jioni walikutana na timu nzima ambapo moja ya jambo walilowasisitizia ni kuhakikisha ushindi wowote unapatikana.
Maximo alisema: “Tunawaheshimu Simba, hii ni mechi ya watani, lakini kwetu tunataka pointi tatu na heshima, tumefanya kila tunalotakiwa kulifanya, timu yangu ina wachezaji bora zaidi ya Simba hivyo nawaomba mashabiki waje kwa wingi kuwaongezea nguvu wachezaji kwani tutaingia kwa akili ya kupambana.”
Wanachama wa Yanga kutoka matawi kadhaa nao wameonekana kuwa mstari wa mbele kwenye maandalizi hayo kwa kuchangishana fedha pamoja na kuipa sapoti kubwa timu yao wakati wa mazoezi. Wanachama wa tawi la Boko walichangishana kiasi cha Sh 1,000,000 ili kusaidia maandalizi ya mchezo huo.
Yanga inaingia kifua mbele kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kuzifunga Prisons ya Mbeya na JKT Ruvu mabao 2-1 kila moja licha ya kipigo chao cha mabao 2-0 ilichopata toka kwa Mtibwa Sugar kwenye mechi ya ufunguzi.
Yanga ina pointi sita kwa sasa ikiwa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara , ipo nyuma ya Mtibwa Sugar na Azam.
Yanga inaweza isibadilishe sana kikosi chake kilichocheza mechi za kwanza.
Kikosi cha leo kinaweza kuwa hivi; langoni atakuwa Deogratias Munishi ‘Dida’, mabeki ni Juma Abdul, Oscar Joshua, Cannavaro na Kelvin Yondani.
Safu ya kiungo itakuwa na Mbuyu Twite, Haruna Niyonzima, Hassan Dilunga, Andrey Coutinho wakati washambuliaji wakiwa ni Genilson Santos ‘Jaja’ na Mrisho Ngassa.
SIMBA
Simba wao waliweka kambi ya siku tisa kule Afrika Kusini ikiwa ni jitihada za uongozi mpya wa timu hiyo chini ya Rais, Evans Aveva, kutaka kupata ushindi kwa namna yoyote ile na kurejesha morali iliyokuwa imepotea kwenye timu kutokana na matokeo yasiyoridhisha kwenye mechi za awali za ligi. Imetoa sare mechi zote tatu za mwanzoni msimu huu.
Kikosi hicho kilifanya mazoezi ya nguvu nchini humo pamoja na kucheza mechi tatu za kujiweka fiti kabla ya kuwakabili watani wao hii leo. Simba ilicheza na Orlando Pirates, University Wits na Jomo Cosmos bila kupata ushindi wowote lakini Phiri amesema mechi hizo zimewajenga vya kutosha kuikabili Yanga.
Kambi hiyo ya Sauzi pia ilihudhuriwa na viongozi kadhaa wa klabu hiyo wakiwemo Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Zacharia Hans Poppe ndiye aliyeongoza msafara huo ambao ulifuatiwa na wapambanaji wengine Makamu wa Kamati hiyo, Kassim Dewji, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Mohamed Nassoro na Makamu wake Idd Kajuna. Viongozi wengine walikuwa Collin Frisch na Said Tulliy.
Kikosi cha Simba kilirejea kwa mafungu juzi Alhamisi na kuelekea moja kwa moja kwenye hoteli ya Golden Tulip jijini Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi yao ya mwisho ambapo mazoezi walikuwa wakifanya kwenye uwanja tulivu wa Gymkhana.
Kwenye mazoezi ya jana Ijumaa, Phiri alionekana kumwandaa kipa Peter Manyika ili awe fiti kwa ajili ya mchezo huo kwa kumpa mazoezi ya kudaka mipira ya krosi pamoja na kudaka penalti. Manyika ana nafasi kubwa ya kuanza kwenye mchezo wa leo baada ya kipa Hussein Sharif ‘Casillas’ kuwa majeruhi wakati Ivo Mapunda akiwa hajapona vizuri kidole alichovunjika wiki tatu zilizopita.
Phiri ambaye anapenda kutumia mfumo wa 4-4-2 ama 3- 5- 2 alisema: “Kwa kawaida mechi ya Simba na Yanga inakuwa ngumu kutokana na upinzani uliopo, ili wanachama na mashabiki wa Simba waweze kufurahi ni lazima uifunge Yanga, hivyo nimekiandaa kikosi changu kwa ajili ya ushindi, naamini wachezaji wangu watafanya vizuri zaidi.
“Wachezaji wote wapo vizuri ukimwacha Casillas na mshambuliaji Raphael Kiongera ambao ni majeruhi, nimewajenga wachezaji wangu kisaikolojia kwani matokeo ya mechi zilizopita sio mazuri. Hakuna mechi tuliyoshinda, zote tumetoka sare hivyo iliwakatisha tamaa.”
Maandalizi ya mechi hiyo yalionekana pia kufanywa na wanachama wa Simba ambapo Mwanaspoti ilizunguka katika baadhi ya matawi na kukuta wanachama wa klabu hiyo wakifanya jitihada za kila aina kuhakikisha timu yao inashinda mechi hiyo ikiwamo kufanya vikao vya mara kwa mara pamoja na mambo ya ufundi wa nje ya uwanja ambayo ni kawaida kwa timu hizi zinapokutana, japo huwa hauna nguvu ya kuleta matokeo mazuri.
Simba itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kutopata ushindi wowote baada ya kutoka sare kwenye mechi zake zote tatu za awali msimu huu. Ilitoka sare ya mabao 2-2 na Coastal Union, kabla ya kutosa sare ya bao 1-1 na Polisi Moro pamoja na Stand United. Kwa sasa Simba inashika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi.
Kikosi cha Simba leo kinatarajiwa kuwa; Kipa Peter Manyika, mabeki William Lucian ‘Gallas’, Issah Rashid ‘Baba Ubaya’, Hassan Isihaka na Joseph Owino.
Viungo ni Jonas Mkude, Ramadhan Singano ‘Messi’, Amri Kiemba na washambuliaji ni Amiss Tambwe, Okwi na Haruna Chanongo.
MECHI NYINGINE WIKIENDI HII
Mbeya City v Azam
Jiji la Mbeya litasimama pia kwa dakika 90 ambapo timu inayopendwa zaidi jijini humo, Mbeya City itakapowakaribisha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Azam FC kwenye mchezo mwingine wa ligi utakaochezwa leo Jumamosi katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini humo.
Mbeya City inaingia kwenye mchezo huo ikiwa inashika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi.
Timu hiyo haijapoteza mchezo wowote mpaka sasa ikiwa imeshinda mechi moja na kutoka sare mara mbili huku ikiwa pia ikiwa timu pekee kwenye ligi ambayo haijaruhusu nyavu zake kutikiswa. Ilitoka Sare tasa na JKT Ruvu na Ruvu Shooting kabla ya kuifunga Coastal Union bao 1-0.
Azam ambayo inatembelea basi ghali zaidi Afrika Mashariki pia ikiongoza kwa utajiri, inaingia kwenye mchezo huo ikiwa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi saba, mbili nyuma ya vinara wa ligi hiyo Mtibwa Sugar. Azam ina kumbukumbu ya sare tasa dhidi ya Prisons kwenye mechi ya mwisho ya ligi.
Awali iliifunga Polisi Moro mabao 3-1 kabla ya kuifunga Ruvu Shooting mabao 2-0.
Coastal Union v Mgambo
Tanga nako kitanuka. Vumbi litatimka kwenye Uwanja wa Mkwakwani ambapo timu mbili kutoka mkoani humo, Coastal Union na Mgambo JKT, zitaonyeshana ubabe kwenye uwanja huo.
Mchezo huo ni miongoni mwa michezo mitatu inayoshirikisha timu zinazotoka mkoa mmoja baada ya ule wa Yanga na Simba na ule wa Mtibwa na Polisi Moro.
Coastal inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi baada ya kuifunga Ndanda ya Mtwara mabao 2-1 kwenye mchezo uliopita. Awali Coastal ilitoka sare ya mabao 2-2 na Simba kabla ya kupoteza kwa Mbeya City ilipofungwa bao 1-0 ugenini.
Mgambo hiyo inaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya vipigo viwili mfululizo baada ya kufungwa bao 1-0 na Stand United na Mtibwa Sugar. Awali timu hiyo iliifunga Kagera Sugar bao 1-0.
Kocha wa Coastal Union, Yusuf Chippo alisema: “Baada ya kupata ushindi wetu wa kwanza morali ya timu imepanda, tumekaa kwa wiki mbili tukirekebisha makosa madogo yaliyojitokeza kwenye mchezo wa mwisho pamoja na kuhimiza mazuri yaendelee, tutapambana kuhakikisha tunapata ushindi mwingine.”
Naye kocha wa Mgambo, Bakari Shime alisema: “Tumekuwa kwenye hali ngumu baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo, tumepambana kurekebisha makosa ili tuweze kupata ushindi kwenye mchezo huo, nina imani wachezaji wangu wanatambua ni nini wanatakiwa kufanya.”
Polisi Moro v Mtibwa
Nyasi za Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro nazo zitawaka moto pale maafande wa Polisi Moro watakapowakaribisha ndugu zao wa Mtibwa Sugar ambao ndio vinara wa ligi kwa sasa.
Mchezo huo unatarajiwa pia kukamata hisia za wapenzi wengi wa soka mkoani Morogoro.
Polisi inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya sare mbili mfululizo na kipigo kimoja.
Ilifungwa mabao 3-1 na Azam kwenye mechi yake ya kwanza kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 na Kagera Sugar na Simba.
Vinara Mtibwa Sugar wao wataingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya kushinda mechi zote tatu za mwanzo na kukaa kileleni mwa msimamo wakiwa na pointi tisa. Iliifunga Yanga mabao 2-0, Ndanda mabao 3-1 na Mgambo bao 1-0.
Kagera v Stand United
Kagera Sugar itakuwa mwenyeji wa Stand United mjini Bukoba katika Uwanja wa Kaitaba.
Kagera itainga uwanjani ikiwa na pointi nne kibindoni baada ya kushinda mchezo mmoja, kupoteza mmoja na kutoka sare mmoja. Ilifungwa bao 1-0 na Mgambo kabla ya kuifunga JKT Ruvu mabao 2-0 na kutoka sare ya bao 1-1 na Polisi Moro.
Stand yenyewe ina kumbukumbu ya sare ya bao 1-1 iliyoipata mbele ya Simba kwenye mchezo wao wa mwisho. Awali timu hiyo ilifungwa mabao 4-1 na Ndanda ya Mtwara kabla ya kuifunga Mgambo bao 1-0.
Ndanda v Ruvu Shooting
Timu ya kwanza kabisa kuongoza ligi msimu huu, Ndanda FC ya Mtwara itakuwa mwenyeji wa maafande wa Ruvu Shooting mchezo utakaochezwa kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Ndanda itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya vipigo viwili mfululizo, ilifungwa mabao 3-1 na Mtibwa Sugar kabla ya kufungwa tena mabao 2-1 na Coastal Union ya Tanga. Awali iliifunga Stand United mabao 4-1.
Ruvu Shooting ina hali mbaya zaidi kwani haijashinda mchezo wowote. Imefungwa mara mbili na kutoka sare moja. Ilichapwa mabao 2-0 na Prisons na ikalala hivyo tena kwa Azam na kutoka sare tasa na Mbeya City.
Prisons v JKT Ruvu
Kesho Jumapili kutakuwa na mchezo mmoja pekee wa ligi hiyo ambapo Prisons ya Mbeya itaikaribisha JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Sokoine.
Prisons itaingia uwanjani ikiwa na pointi nne baada ya kushinda mchezo mmoja, kupoteza mmoja na kutoka sare moja. Iliifunga Ruvu Shooting mabao 2-0 kabla ya kufungwa mabao 2-1 na Yanga na kisha kutoka sare tasa na Azam.
JKT Ruvu ina pointi moja pekee ikiwa imefungwa mechi mbili na kutoka sare mara moja. Ilitoka sare tasa na Mbeya City kabla ya kufungwa mabao 2-0 na Kagera Sugar na kisha mabao 2-1 na Yanga.