Ninje ayakumbuke haya

Muktasari:
Kutokana na cheo alichonacho Ammy Ninje cha Ukurugenzi wa Ufundi wa TFF, anatakiwa kuwafuatilia makocha wote wazawa ambao wanafundisha ndani na nje ya nchi ili kuwa na mawasiliano mazuri ambayo yatakuwa na manufaa kuendeleza wachezaji wazawa hata soka la vijana.
SHIRIKISHO la soka Tanzania (TFF) lilimtangaza Ammy Ninje kuwa Mkurugenzi wa Ufundi mara baada ya kumuondoa Oscar Milambo ambaye alikuwa akikaimu nafasi hiyo.
Ninje ambaye kabla ya kuwa katika nafasi hiyo alifundisha timu mbalimbali za Taifa hapa nchini kama Taifa Stars akisaidiana na Salum Mayanga, Kilimanjaro Heroes na Serengeti Boys.
Hivi karibuni, Ninje aliwasili nchini akitokea Uingereza ambako alikuwa anaishi na kuanza kibarua chake cha Ukurugenzi wa Ufundi. Makala haya inakuletea baadhi ya majukumu ambayo anatakiwa kuanza nayo.
MIPANGO TIMU ZA VIJANA
Ninje miongoni mwa majukumu aliyokuwa nayo na huenda litakuwa la kwanza anatakiwa kulifanyia kazi ni mipango endelevu katika soka la vijana ambayo ni kiini cha wachezaji soka kilipo.
Ili afanikiwe kwenye mipango endelevu soka la vijana kufanya mafunzo yenye vigezo vya makocha ambao watakuwa na sifa za kutafuta vijana wenye vipaji kuwazalisha na kuwatunza ili kukuwa katika njia sahihi.
Anatakiwa kubuni mashindano ya vijana mengi ambayo ni endelevu kama ilivyokuwa awali ya Copa Cocacola, Uhai na mengine mengi.
Kuwepo na mipango endelevu ya kufundisha madaktari, waamuzi na mafunzo mengine yatakayolenga kukuza soka la vijana pamoja na kuwepo na njia sahihi ya kuwapata hao waamuzi.
Katika nafasi yake anatakiwa kuweka vigezo stahiki na sahihi kwa waamuzi ambao watakuwa na jukumu la kuchezesha mechi za Ligi Kuu na si kuwepo wale ambao hawana vigezo na kwenda kufanya maamuzi ambayo si sahihi na mwisho wake kufungiwa.
KANUNI BORA ZA LIGI
Ninje katika nafasi yake anatakiwa kuweka kanuni bora za mashindano ya ligi zote ambazo zinatambuliwa na Shirikisho la soka Afrika (CAF) miongoni mwa hizo zinatakiwa kulenga soka la vijana.
Kila klabu inatakiwa kuwa na leseni ambazo miongoni mwake Ninje na kamati yake ndio wataweka kanuni za ligi kama idadi ya wachezaji wa kigeni ambao wanatakiwa kuwepo katika timu na ambao wanatakiwa kutumika katika mechi husika.
Kuweka kanuni na sheria ya idadi za klabu zinazotakiwa kuwepo katika ligi na si maamuzi ya kuongeza au kupunguza timu ili kusaidia kuwapata wadhamini ambao wataweza kuwekeza.
Kama timu zikiwa zinaongezwa au kupunguzwa bila kuwepo na kanuni ambazo zitakuwa hazishirikiani na wadhamini wenyewe ligi inaweza kuwa kama msimu mpaka wakati hii haina udhamini huenda kuongezeka kwa timu msimu huu ilichangia.
KUANDAA MIFUMO KAMILI
Ninje anatakiwa kuandaa mifumo ambayo itakuwa inawafuatilia makocha wote wa timu za Taifa ambao watakuwa wakifanya kazi chini yake na kuweka mipango mikakati ya muda mrefu na mfupi.
Mkurugenzi wa ufundi katika klabu au nchi anakuwa na nafasi ya kuchagua au kupendekeza makocha ambao wanatakiwa kuifundisha timu kubwa za Taifa au zile za vijana.
Makocha wote wa timu za Taifa wanatakiwa kuwa wanaripoti kwake kila ambacho watakuwa wanafanya lakini Ninje atakuwa na uwezo kumpangia programu za kufanya makocha wote.
KUENDESHA TIMU ZA TAIFA
Mkurugenzi atakuwa na nafasi ya kubuni njia sahihi ya kuendesha timu zote za Taifa kama muda wa kuweka kambi kwani katika dunia ya sasa ni nchi chache ambazo zinatumia siku10.
Kutambua na kuelewa ratiba ya Shirikisho la soka Afrika (CAF) na si kuona ligi ya ndani inasimama sababu ikiwa ni kuingiliana kwa ratiba jambo hilo kwa sasa linaisumbua zaidi ligi ya Tanzania Bara.
Ninje anatakiwa kufahamu kila aliyekuwa katika nafasi ya uongozi kwenye timu za Taifa ana uweledi na sifa za kukaa sehemu hiyo, kwa mfano kama daktari wa timu anatakiwa kuwa kweli na taaluma hiyo na hata waliokuwa kwenye nafasi nyingine kama Meneja, Mtunza vifaa, hata kocha wa timu za Taifa wote wawe na taaluma husika.
MAKOCHA WA KLABU
Ninje anatakiwa kubuni na kuwepo na sheria ambazo makocha wa klabu kuwa na sifa stahiki kwenye benchi hilo na hata wale ambao watakuwa wanakaimu kuwa na muda husika usiopita siku 60.
Mkurugenzi wa ufundi na kamati yake anatakiwa kuanzisha utaratibu wa makocha wote wa timu za Ligi Kuu Bara kukutana kila baada ya ligi kumalizika ili kutoa tathmini yao ya kile walichokiona.