Nidhamu yambeba Banda Sauzi

Muktasari:
Banda ameichezea Baroka michezo 22 ya Ligi Kuu Afrika Kusini ‘PSL’huku pia akihusika mwenye michezo mingine isiyopungua minne ya kombe la Ligi ‘FA’ nchini humo na yote hiyo hajui kadi ni nini.
SOKA bila kadi, linawezekana. Ndio. Kama unabisha basi msikie mwenyewe beki wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga na Baroka FC ya Afrika Kusini, Abdi Banda. Anakuambia hajawahi kupata kadi hata moja ya njano tangu atue klabuni hapo akitokea Simba.
Banda ameichezea Baroka michezo 22 ya Ligi Kuu Afrika Kusini ‘PSL’huku pia akihusika mwenye michezo mingine isiyopungua minne ya kombe la Ligi ‘FA’ nchini humo na yote hiyo hajui kadi ni nini.
“Yeah!! Sijawahi kupata kadi ya njano, nimekuwa nikijitahidi kucheza kwa nidhamu, sisemi kama nitamaliza msimu bila ya kupata kadi, lakini kama nikifanya hivyo itakuwa rekodi kwangu.
“Kwa uchezaji wangu huu kwa Tanzania nilikuwa napata sana kadi, kwa sasa kiasi fulani najiona kubadilika, nacheza tafu lakini kinidhamu sio kwa kukurupuka bila mpango,” alisema.
Kuhusu ubora wa timu ya Taifa, Taifa Stars, beki huyo wa zamani wa Simba ya Dar es Salaam na Coastal Union ya Tanga alisema kama idadi ya wachezaji wa Kitanzania wanaocheza nje ya nchi ikiendelea kuongezeka ni wazi Taifa Stars itatisha kwa siku za usoni.