NI LOS ANGELES LAKERS VS MIAMI HEAT FAINALI NBA

Monday September 28 2020
kikapu pic

HATIMAYE fainali ya ligi maarufu ya kikapu Marekani (NBA) na duniani kwa ujumla, itazishuhudia timu za Los Angeles Lakers dhidi ya Miami Heat zilizofanikiwa kushinda fainali za kanda zao.

Los Angeles Lakers ilikuwa ya kwanza kukata tiketi ya kucheza fainali ya NBA baada ya kuiondosha timu iliyofanya maajabu msimu huu, Denver Nuggets, ndani ya mechi tano pekee.

Ushindi wa pointi 117 dhidi ya 107 za Denver Nuggets jana Jumapili, uliwapa Lakers matokeo ya 4-1 na kuendeleza rekodi ya Lakers kwenye hatua ya mtoano (Playoffs), kwani awali ilizitoa Portland Trail Blazers na Houston Rockets kwa matokeo hayo hayo ya 4-1 ikiwa ni mechi tano badala ya saba za kuamua mshindi.

Supastaa wa timu hiyo, LeBron James aliwahakikishia Lakers kucheza fainali yao ya kwanza tangu timu hiyo ilipocheza fainali hiyo mwaka 2010, LeBron alifunga triple-double yake ya pili kwenye mtoano, pointi 38, ribaundi 16 na asisti 10, akifikisha 27 kwa ujumla alizoandikisha kwenye playoffs.

Leo asubuhi, Miami Heat kwa upande wao, wakiongozwa na Jimmy Butler, wameiondosha Boston Celtics kwenye mchezo wa sita kwa matokeo ya 4-2 kufuatia ushindi wa pointi 125-113 za Celtics waliokuwa wanasaka taji lao la 18 wakiwa wanaongoza kwa kubeba mara 17.

Nyota Bam Adebayo ndiye aliyeongoza kichapo cha Celtics leo kufuatia kufunga kwake pointi 32 ambazo ni rekodi kwake pamoja na ribaundi 14 na asisti tano, akiwafunga mdomo waliomlaumu mchezo wa tano waliopoteza.

Advertisement

Fainali ya kuwania taji la NBA sasa itaanza Alfajiri ya Alhamisi wiki hii, ambapo Los Angeles Lakers wakuwa na shughuli pevu ya kulitwaa taji hilo baada ya miaka 10, huku Miami Heat wao wakiwa wanalisaka miaka sita tangu walipobeba mara ya mwisho mwaka 2014.

Advertisement